
Jumuiya ya Qur’ani ya Oman iliandaa awamu ya nne ya maadhimisho ya kila mwaka ya Siku ya Qur’ani katika Msikiti na Baraza la Bibi Fatima al-Zahra (Amani iwe juu yake - SA), uliopo katika Mji wa Sultan Qaboos, Jimbo la Bawshar.
Kwa mujibu wa gazeti la Al-Sharq, tukio hilo liliandaliwa kwa ushiriki wa takriban watu 600 wa rika zote. Siku ya Qur’ani nchini Oman ni tukio la kila mwaka linalofanyika nchi nzima likiratibiwa na Jumuiya ya Qur’ani ya Oman.
Maadhimisho haya ni programu maalum na ya kina ya Qur’ani ambapo washiriki husoma Qur’ani nzima au sehemu walizohifadhi mbele ya mwalimu (Ustadh) anayesikiliza na kusahihisha kwa umakini.
Sehemu mahususi ya programu hiyo imetengwa kwa ajili ya usomaji wa Qur’ani, ikifanyika katika mazingira yenye hamasa na ushindani wa kiroho kwa muda wa siku nzima. Awamu hii ya nne ya Siku ya Qur’ani ya Oman, iliyojikita zaidi katika masuala ya hifdhu, ilijumuisha vitengo kadhaa kama vile: kuhifadhi Qur’ani nzima, Juzuu 20, Juzuu 15, Juzuu 10, Juzuu 5, Juzuu 3, na Juzuu 2.
Maadhimisho hayo yalifikia tamati kwa kuwatuza na kuwapa heshima Mahafidh waliohitimisha Qur’ani nzima, pamoja na walimu waliojitolea kusikiliza masomo hayo na vijana wajitoleaji waliofanikisha shughuli hiyo kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
3497583