IQNA

Video ya Rais Erdoğan akisoma Qur’ani yatikisa mitandao ya kijamii

21:37 - May 31, 2026
Habari ID: 3482306
IQNA – Video iliyosambazwa mtandaoni ikimuonesha Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, akisoma aya za Qur’ani Tukufu ndani ya Msikiti wa Aya Sofya mjini Istanbul, imepokelewa vyema na watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Usomaji huo ulifanyika wakati wa hafla iliyoandaliwa kuadhimisha kumbukumbu ya ushindi wa kuiteka Konstantinopoli mwaka 1453, kwa mujibu wa duru ya habari ya El-Balad.

Msikiti wa kihistoria wa Aya Sofya ulikuwa mwenyeji wa kisomo hicho, ambacho kilikuja sambamba na maadhimisho ya kitaifa ya mwaka wa 573 tangu kutekwa kwa Konstantinopoli.

Msikiti huo ni miongoni mwa alama muhimu zaidi za kihistoria nchini Uturuki, na umepitia mabadiliko mengi katika vipindi mbalimbali vya historia, hadi ulipofunguliwa tena rasmi kama msikiti mwaka 2020 baada ya kutumika kwa miaka kadhaa kama makumbusho.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii walisambaza video na vipande vya matukio vilivyoonesha nyakati za kiroho wakati Erdoğan alipokuwa akisoma aya za Qur’ani katika mazingira yenye utulivu na utukufu ndani ya Msikiti wa Aya Sofya. Video hiyo ilivutia hisia na umakini mkubwa wa umma.

Katika kisomo chake, Erdoğan alijikita katika Surat al-Baqarah, kwa kuzingatia undani na uzito wa maana za aya alizosoma.

Kipande hicho cha video cha rais wa Uturuki akisoma Qur’ani Tukufu kilizua hisia na mijadala mbalimbali mtandaoni, huku wakati huo wa kisomo ukipata sifa nyingi na zaidi ya miitikio milioni mbili katika majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Watumiaji wengi wanaamini kuwa hamasa ya kiongozi huyo wa Uturuki kusoma Qur’ani katika mahali hapo patakatifu inatuma ujumbe wa wazi kuhusu kushikamana na utambulisho wa Kiislamu pamoja na urithi wa kihistoria.

3497659

captcha