IQNA

Shahidi Imam Khamenei kuzikwa katika Haram ya Imam Ridha (AS) tarehe 9 Julai, mamilioni kushiriki

17:31 - June 13, 2026
Habari ID: 3482354
IQNA-Ofisi inayohusika na kuhifadhi na kuchapisha kazi za Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza ratiba ya hafla za kuaga, mazishi, na kuzikwa kwa Shahidi Ayatullah Imam Sayyid Ali Khamenei ambapo mamilioni wanatarajiwa kushiriki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo, hafla za kuaga mwili wa Kiongozi Shahidi zitafanyika katika Msala wa Imam Khomeini mjini Tehran tarehe 4 na 5 Julai, zinazolingana na tarehe 19 na 20 za mwezi wa Muharram.

Msafara wa mazishi mjini Tehran umepangwa kufanyika tarehe 6 Julai, huku msafara mwingine wa mazishi ukitarajiwa kufanyika katika mji mtukufu wa Qom tarehe 7 Julai.

Hafla ya mwisho ya mazishi itafanyika katika mji mtukufu wa Mashhad tarehe 9 Julai, sambamba na mkesha wa kumbukumbu ya shahada ya Imam Sajjad (AS). Taarifa hiyo imeeleza kuwa Kiongozi Shahidi atazikwa katika Haram tukufu ya Imam Ridha (AS).

Waandalizi wamewaalika “watu wote watukufu na wapendwa, watu huru wa dunia, wafuasi wa madrasah ya Uislamu, na wote wanaoipenda Iran” kushiriki katika hafla hizo na kutoa heshima za mwisho kwa Kiongozi Shahidi.

Taarifa hiyo pia imezishukuru taasisi za serikali na makundi ya wananchi kwa maandalizi makubwa yaliyofanywa, ikisisitiza kuwa jukumu kuu katika kuandaa hafla hizo litakuwa mikononi mwa wananchi wenyewe kama “wamiliki halisi wa maombolezo,” na kuongeza kuwa ushiriki wa watu kwa kiwango kisicho na mfano unatarajiwa.

Maelezo zaidi kuhusu hafla hizo yatatangazwa baadaye.

Mji wa Mashhad wajitayarisha kupokea mamilioni

Wakati huo huo, mji mtakatifu wa Mashhad umeanza maandalizi ya kuwakaribisha takriban waombolezaji milioni kumi watakaohudhuria mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khamenei.

Gholamhossein Mozaffari, gavana wa mkoa wa Khorasan Razavi ulioko kaskazini mashariki mwa Iran, alitangaza hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Mashhad siku ya Ijumaa. Amesema mipango ya kina imeanza kwa ajili ya maandalizi ya ibada ya mazishi na maziko ya Kiongozi huyo shahidi katika mji huo mtakatifu.

Akisisitiza utayari kamili wa mkoa huo kuwahudumia idadi kubwa ya washiriki, alisema uwezo wote wa kiutendaji, huduma, usalama na rasilimali za umma katika Khorasan Razavi utawekwa kazini ili kuhakikisha hafla hiyo inafanyika kwa utaratibu mzuri na kwa hadhi inayostahili.

Alieleza kuwa tangu kutangazwa kwa mahali pa maziko, mikutano mingi ya uratibu imeanza kufanyika katika ngazi ya mkoa, huku taasisi mbalimbali za utendaji, huduma, uokoaji, utekelezaji wa sheria na vyombo vya usalama zikijiandaa kuweka mazingira yanayofaa kwa ajili ya kuwahudumia mahujaji na washiriki wa hafla hiyo.

Akibainisha kuwa kati ya watu milioni 8 hadi 10 wanatarajiwa kuhudhuria, Mozaffari alisema kusimamia idadi hiyo kubwa kunahitaji mipango makini katika sekta za usafiri, malazi, huduma za miji, afya, matibabu, uokoaji na usalama. Kwa sababu hiyo, mikutano mingi maalumu ya kitaalamu imefanyika katika ngazi za mkoa na taifa.

Gavana wa Khorasan Razavi pia alisisitiza uzoefu wa mkoa huo katika kuandaa mikusanyiko mikubwa ya kitaifa na kidini. Alisema mji wa Mashhad katika miongo iliyopita umekuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kitaifa mara nyingi, na una uwezo mkubwa wa kijamii na kiutawala wa kusimamia matukio ya aina hiyo.

Kwa mujibu wake, uratibu unaendelea pia kufanywa na taasisi za kitaifa ili kuhakikisha mahujaji wanapata huduma kwa urahisi na kwa changamoto chache iwezekanavyo.

Mozaffari aliongeza kuwa kufanyika kwa mazishi ya Kiongozi Shahidi kutatoa fursa ya kuonesha mshikamano wa kitaifa, umoja wa kijamii na uwezo wa kiutendaji wa mkoa wa Khorasan Razavi, huku taasisi zote zikijitahidi kuhakikisha hafla hiyo inafanyika kwa njia bora zaidi.

Aidha, alisema kuwa mbali na umuhimu wake wa kiroho, tukio hilo linaweza pia kuonesha uwezo wa kitamaduni, kijamii na kiutawala wa mkoa huo.

Ayatullah Khamenei aliuawa shahidi na majeshi ya kigaidi ya Marekani na Israel katika makazi yake mjini Tehran tarehe 28 Februari, wakati tawala hizo mbili zilipoanzisha vita vya uchokozi dhidi ya Iran ambavyo pia vilishuhudia kuuawa kwa makamanda kadhaa wa juu wa kijeshi.

Siku chache baadaye, Baraza la Wataalamu la Iran, chombo chenye wanazuoni 88 wa Kiislamu, lilimchagua Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei mwenye umri wa miaka 56 kuwa Kiongozi wa tatu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei ni mwana wa Shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Ikumbukwe kuwa Shahidi Imam Khamenei aliuawa katika hujuma ya kigaidi ya Marekani na Israel mnamo 10 Ramadhani sawa na 28 Februari mwaka huu katika siku ya kwanza ya vita vilivyoendelea kwa muda wa siku 40.

3497824

captcha