
Katika ujumbe huo uliotolewa Alhamisi, Kiongozi Muadhamu ametilia mkazo umuhimu wa mchango wa wananchi na mahudhurio yao katika medani na kusema: Wananchi wanataka kuendelezwa mapambano athirifu na ya kumjutisha adui.
Katika ujumbe huo, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei ametoa shurani zake za dhati kwa wapiganaji shupavu wa Iran ambao wamefunga njia ya uvamizi wa adui na mipango yake ya kutaka kuigawa Iran kwa kutoa vipigo murua kwa maadui. Vilevile amewashukuru wapiganaji wa Kambi ya Muqawama akisema kambi ya Muqawama ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na thamani na maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Shirika la Habari la Hawza, limechapisha matini kamili ya ujumbe huo ifuatavyo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
مَا نَنسَخْ مِنْ ءَآیَةٍ أَوْ نُنسِهَا نَأتِ بِخَیْرٍ مِّنْهَآ اَوْ مِثْلِها.
اَلسَّلامُعَلَیکَ یا داعِیَاللهِ وَ رَبّانِیَّ آیاتِهِ،
اَلسَّلامُعَلَیکَ یا بابَاللهِ وَ دَیّانَ دینِهِ،
اَلسَّلامُعَلیکَ یا خَلیفَةَاللهِ و ناصِرَ حَقِّهِ،
اَلسَّلامُعَلیکَ یا حُجَّةَاللهِ وَ دَلیلَ اِرادَتِه؛
اَلسَّلامُعَلیکَ اَیُّهَا المُقَدَّمُ المَأمُول؛
اَلسَّلامُعَلیکَ بِجَوامِعِ السَّلام؛
اَلسّلامُعَلیکَ یا مَولایَ صاحِبَ الزَّمان.
“Hatufuti aya yoyote wala kuifanya isahaulike isipokuwa tunaleta iliyo bora zaidi kuliko hiyo au mfano wake.”Amani iwe juu yako ewe mwitaji wa Mwenyezi Mungu na mlezi wa aya zake;
Amani iwe juu yako ewe mlango wa Mwenyezi Mungu na msimamizi wa dini yake;
Amani iwe juu yako ewe khalifa wa Mwenyezi Mungu na msaidizi wa haki yake;
Amani iwe juu yako ewe hoja ya Mwenyezi Mungu na dalili ya mapenzi yake;
Amani iwe juu yako ewe mtangulizi anayetegemewa;
Amani iwe juu yako kwa aina zote za salamu;
Amani iwe juu yako ewe mola wangu, Imam wa zama (Sahib az-Zaman).
Mwanzoni mwa maneno yangu ninapaswa kumpa pole bwana Imam wa Zama, Mwenyezi Mungu aiharakishe faraja yake, kwa tukio la kusikitisha la kuuawa kishahidi Kiongozi mtukufu wa Mapinduzi, Khamenei mpendwa na mwenye hekima. Pia ninaomba dua njema kutoka kwake kwa kila mmoja wa watu wa taifa kubwa la Iran, na hata kwa Waislamu wote duniani, kwa wahudumu wote wa Uislamu na Mapinduzi, kwa wanaojitolea na kwa waliobaki nyuma ya mashahidi wa harakati ya Kiislamu, hasa wa vita vya hivi vya karibuni, na pia kwa ajili yangu mimi mnyonge.
Sehemu ya pili ya maneno yangu inaelekezwa kwa taifa kubwa la Iran. Kwanza kabisa, ninapaswa kueleza kwa ufupi msimamo wangu kuhusu kura ya Baraza tukufu la Wanazuoni Wataalamu. Mimi mtumishi wenu, Sayyid Mujtaba Husayni Khamenei, kama ninyi pia, nilipata habari ya matokeo ya kura ya baraza hilo kupitia runinga ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa upande wangu, kuketi mahali ambapo hapo awali waliketi viongozi wawili wakubwa, Khomeini Mkuu na Khamenei Shahidi , ni jambo gumu. Kwa sababu kiti hiki kilikaliwa na mtu ambaye baada ya zaidi ya miaka 60 ya mapambano katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuacha aina zote za starehe na ladha za dunia, alibadilika kuwa johari inayong’aa na sura ya kipekee sio tu katika zama hizi bali katika historia yote ya watawala wa nchi hii. Maisha yake na hata namna ya kifo chake vilijaa utukufu na heshima iliyotokana na kumtegemea Mwenyezi Mungu.
Nilipata heshima ya kuuona mwili wake baada ya kuuawa shahidi. Nilichokiona kilikuwa ni mlima wa uimara; na nikaambiwa kwamba mkono wake mzima ulikuwa umefinywa kwa nguvu katika ngumi. Kuhusu nyanja mbalimbali za utu wake, wenye maarifa wanapaswa kuzungumza mengi kwa muda mrefu. Katika nafasi hii nitatosheka na muhtasari huu na kuacha maelezo kwa fursa nyingine zinazofaa. Hii ndiyo sababu ya ugumu wa kuketi kwenye kiti cha uongozi baada ya mtu kama huyo. Kujaza pengo hili kunawezekana tu kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na kwa msaada wenu nyinyi wananchi.
Katika kuendelea, ni lazima nisisitize jambo ambalo lina uhusiano wa moja kwa moja na msingi wa maneno yangu.
Jambo hilo ni kwamba mojawapo ya ustadi wa kiongozi shahidi na mtangulizi wake mkubwa ilikuwa ni kuwaingiza watu katika nyanja zote, kuwapa mwamko na ufahamu wa kudumu, na katika utekelezaji wa mambo kutegemea nguvu yao. Kwa njia hii walifanya maana halisi ya “umma” na “jamuhuri” iwe hai, na walikuwa wanaamini hilo kwa dhati kabisa.
Matokeo ya wazi ya jambo hili yalionekana katika siku hizi chache ambazo nchi ilikuwa bila kiongozi na bila Amiri Jeshi Mkuu. Uelewa na busara ya taifa kubwa la Iran katika tukio la hivi karibuni, pamoja na uthabiti, ujasiri na uwepo wao, uliwafanya marafiki kuwapongeza na maadui kushangaa. Ni nyinyi wananchi mlioongoza nchi na kuhakikisha nguvu yake.
Aya niliyotaja mwanzoni mwa maandishi haya ina maana kwamba hakuna aya yoyote ya Mwenyezi Mungu inayofutwa au kusahaulika isipokuwa kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu huweka mahali pake mfano wake au iliyo bora zaidi.
Sababu ya kutumia aya hii si kwamba mimi mtumishi wenu niko katika kiwango cha kiongozi shahidi, sembuse kudhaniwa kuwa bora kuliko yeye,bali kusudi ni kuonesha nafasi sahihi na muhimu yenu nyinyi taifa pendwa. Ikiwa neema ile kubwa iliondolewa kutoka kwetu, badala yake uwepo wa taifa la Iran kwa namna madhubuti umepewa tena mfumo huu. Mfahamu hili: ikiwa nguvu yenu haitadhihirika uwanjani, si uongozi wala taasisi nyingine zozote — ambazo jukumu lao halisi ni kuwahudumia wananchi — hazitakuwa na ufanisi unaohitajika.
Ili maana hii ipate uhalisia:
Kwanza, kumkumbuka Mwenyezi Mungu Mtukufu, kumtegemea Yeye na kushikamana na nuru za watoharifu (Maasumina) , rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao, kunapaswa kuangaliwa kama dawa kuu na nguvu ya kipekee inayohakikisha kufunguliwa milango ya mafanikio na ushindi wa hakika dhidi ya adui. Hii ni faida kubwa ambayo nyinyi mnayo na maadui wenu hawana.
Pili, umoja kati ya watu na makundi mbalimbali ya taifa, ambao kawaida hujitokeza zaidi wakati wa shida, haupaswi kuharibiwa. Hili litapatikana kwa kupuuza mambo yanayoweza kuleta mgawanyiko.
Tatu, uwepo madhubuti katika uwanja lazima udumishwe; iwe kwa namna mlivyoonyesha katika siku na usiku wa vita hivi, au kwa aina mbalimbali za mchango katika nyanja za kijamii, kisiasa, kielimu, kitamaduni na hata kiusalama. Kilicho muhimu ni kuelewa vizuri jukumu sahihi bila kuharibu umoja wa kijamii na kulitekeleza kadiri iwezekanavyo. Moja ya majukumu ya uongozi na baadhi ya viongozi wengine ni kuwakumbusha watu majukumu haya. Kwa sababu hiyo ninakumbusha umuhimu wa kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Quds ya mwaka 1447, ambapo kipengele cha kuvunja nguvu ya adui kinapaswa kupewa umuhimu na wote.
Nne, msiache kusaidiana. Kwa rehema za Mwenyezi Mungu, tabia ya watu wengi wa Iran daima imekuwa hivyo, na inatarajiwa kwamba katika siku hizi maalum , ambazo kwa kawaida ni ngumu zaidi kwa baadhi ya watu , jambo hili litadhihirika zaidi. Hapa pia ninaomba taasisi za huduma zitoe msaada wowote kwa wananchi hawa wapendwa na kwa miundo ya kijamii ya misaada bila kusita.
Ikiwa mambo haya yatazingatiwa, njia ya kufikia siku za utukufu na fahari kwa taifa lenu itakuwa rahisi. Mfano wa karibu zaidi unaweza kuwa, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, ushindi dhidi ya adui katika vita vya sasa.
Sehemu ya tatu ya maneno yangu ni shukrani za dhati kwa wapiganaji wetu mashujaa ambao, katika hali ambapo taifa letu na nchi yetu pendwa imeshambuliwa kwa dhuluma na viongozi wa kambi ya ubeberu, kwa mapigo yao makali wamezuia njia ya adui na kuwatoa katika dhana ya uwezekano wa kutawala nchi yetu au hata kuigawa.
Ndugu wapiganaji wapendwa!
Matakwa ya watu ni kuendelea kwa ulinzi wenye athari na wenye kumfanya adui ajute. Pia, bila shaka, chombo cha kufunga Mlango wa Hormuz kinapaswa kuendelea kutumika. Kuhusu kufungua medani nyingine ambazo adui ana uzoefu mdogo nazo na ambazo atakuwa dhaifu sana ndani yake, tafiti zimefanywa na kuanzishwa kwake kutatekelezwa ikiwa hali ya vita itaendelea na kwa kuzingatia maslahi.
Pia ninawashukuru kwa dhati wapiganaji wa Jabhatu-l-Muqawama (Mrengo wa Muqawama). Tunaziona nchi za mrengo wa muqawama kama marafiki wetu bora, na suala la muqawama ni sehemu isiyotenganishwa na maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Bila shaka, ushirikiano wa vipengele vya kambi hii utapunguza muda wa kuondokana na fitina ya Kizayuni. Kama tulivyoona, Yemen shujaa na mwenye imani hakuacha kuwatetea watu waliodhulumiwa wa Ghaza, na Hizbullah mwenye kujitoa licha ya vikwazo vyote amekuja kusaidia Jamhuri ya Kiislamu; pia muqawama wa Iraq umechukua mstari huo huo kwa ujasiri.
Sehemu ya nne ya maneno yangu, inaelekezwa kwa wale waliopata madhara katika siku hizi chache zilizopita: iwe ni wale waliopoteza wapendwa wao kwa shahada, au waliojeruhiwa, au wale ambao nyumba zao au biashara zao zimeharibiwa.
Kwanza, ninatoa pole zangu za dhati kwa familia za mashahidi watukufu. Hili linatokana na uzoefu wa pamoja nilio nao na watu hawa watukufu. Mbali na baba yangu ambaye kuondoka kwake limekuwa jambo la taifa zima, nimemtoa pia mke wangu mpendwa na mwaminifu ambaye nilikuwa na matumaini mengi kwake; dada yangu mwenye kujitolea aliyekuwa akiwahudumia wazazi wake hadi akapata malipo yake; pamoja na mtoto wake mdogo; na pia shemeji yangu ambaye alikuwa mtu mwenye elimu na heshima — wote wamejiunga na msafara wa mashahidi.
Lakini kinachofanya subira iwezekane hata iwe rahisi katika misiba ni kuzingatia ahadi ya Mwenyezi Mungu ya malipo makubwa kwa wenye kusubiri. Hivyo lazima tuvumilie na tumtegemee Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa matumaini na uaminifu.
Pili, ninawahakikishia wote kwamba; hatutasamehe kisasi cha damu ya mashahidi wenu. Kisasi tunachokusudia hakihusiani tu na shahada ya kiongozi mkuu wa Mapinduzi; bali kila mwananchi anapouawa kishahidi na adui ni faili jipya la kisasi. Sehemu ndogo ya kisasi hiki tayari imeonekana, lakini hadi ifikie kiwango chake kamili faili hii itaendelea kuwa juu ya faili nyingine zote. Hasa tutakuwa na hisia kubwa zaidi kuhusu damu ya watoto wetu. Kwa hiyo uhalifu ambao adui alifanya kwa makusudi dhidi ya Shule ya Shajarat Taybah ya Minab na matukio kama hayo yatachunguzwa kwa umuhimu maalum.
Tatu, waliojeruhiwa katika mashambulizi haya lazima wapate huduma za matibabu zinazofaa bila malipo na kufaidika na baadhi ya manufaa mengine.
Nne, kadiri hali ya sasa inavyoruhusu, hatua za kutosha zinapaswa kuchukuliwa kufidia hasara za mali kwa nyumba na mali binafsi. Mambo haya mawili ya mwisho ni wajibu wa lazima kwa viongozi husika ambao wanapaswa kuyatekeleza na kunipa taarifa.
Jambo moja ninalopaswa kusisitiza ni hili: kwa vyovyote vile tutachukua fidia kutoka kwa adui; na ikiwa atakataa, tutachukua kutoka katika mali zake kwa kiwango tutakachoona kinafaa; na ikiwa hilo pia halitawezekana, basi tutaharibu mali zake kwa kiwango hicho hicho.
Sehemu ya tano ya maneno yangu, inaelekezwa kwa viongozi na watu wenye ushawishi katika baadhi ya nchi za eneo hili. Tuna mipaka ya nchi kavu au bahari na nchi 15, na daima tumekuwa tukitaka uhusiano mzuri na wa kujenga na wote. Lakini kwa miaka mingi adui ameanzisha hatua kwa hatua vituo mbalimbali vya kijeshi na kifedha katika baadhi ya nchi hizi ili kuimarisha udhibiti wake wa eneo hili.
Katika shambulio la hivi karibuni, baadhi ya vituo vya kijeshi vilitumika; hivyo basi, kama tulivyokuwa tumetoa onyo wazi, bila kushambulia nchi hizo, tulilenga tu vituo hivyo. Kuanzia sasa, kwa kulazimika, tutalazimika kuendelea kufanya hivyo, ingawa bado tunaamini katika umuhimu wa urafiki kati yetu na majirani zetu.
Nchi hizi zinapaswa kubainisha msimamo wao kuhusu wale wanaovamia nchi yetu na wanaoua wananchi wetu. Ninapendekeza wafunge vituo hivyo haraka iwezekanavyo, kwa sababu bila shaka sasa wameelewa kwamba madai ya Marekani ya kuleta usalama na amani yalikuwa uongo.
Hatua hii itawafanya wawe karibu zaidi na mataifa yao wenyewe, ambayo kwa kawaida hayaridhiki na kushirikiana na kambi ya ukafiri na tabia yake ya kudhalilisha.
Tunarudia tena: mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu uko tayari kabisa kwa umoja na uhusiano wa karibu na majirani wote bila kutafuta ukoloni au utawala katika eneo hili.
Sehemu ya sita ya maneno yangu inaelekezwa kwa kiongozi wetu shahidi.
Ewe kiongozi! Kwa kuondoka kwako umeacha majonzi makubwa katika nyoyo za wote. Daima ulitamani mwisho huu, na hatimaye Mwenyezi Mungu akakupa katika hali ya kusoma Qur’ani Tukufu asubuhi ya siku ya kumi ya Ramadhani.
Ulivumilia dhuluma nyingi kwa utulivu na nguvu bila kuonesha udhaifu. Wengi hawakutambua thamani yako halisi, na pengine itachukua muda mrefu hadi pazia mbalimbali ziondoke na baadhi ya ukweli uonekane.
Tunatumaini kwamba; kutokana na daraja lako la karibu na watakatifu, waaminifu na mashahidi, utaendelea kufikiria maendeleo ya taifa hili na mataifa yote ya kambi ya muqawama na kuwaombea,kama ulivyokuwa ukifanya katika maisha yako ya duniani. Tunakuahidi kwamba tutafanya kila juhudi kuinua bendera hii , ambayo ni bendera kuu ya kambi ya haki , na kufikia malengo yako matakatifu.
Katika sehemu ya saba, ninawashukuru watu wote walioniunga mkono mimi, wakiwemo Mara'ji' wakuu wa dini na watu mbalimbali wa kitamaduni, kisiasa na kijamii, pamoja na wananchi ambao wamehudhuria mikusanyiko mikubwa kuonesha upya utii wao kwa mfumo huu. Pia ninawashukuru viongozi wa mihimili mitatu ya serikali na Baraza la Muda la Uongozi kwa mipango na hatua zao nzuri.
Natumaini rehema maalum za Mwenyezi Mungu katika siku na nyakati hizi zenye baraka ziwafikie watu wote wa Iran na hata Waislamu wote na wanyonge duniani.
Mwisho kabisa, namuomba bwana wetu (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) katika masiku haya yaliyosalia ya usiku na siku za Laylatul-Qadr na mwezi mtukufu wa Ramadhani, amuombe Mwenyezi Mungu Mtukufu awape watu wetu ushindi wa wazi dhidi ya adui, pamoja na heshima, upanuzi na afya, na kwa waliotangulia mbele ya haki awape daraja za juu na rehema za Akhera.
Amani iwe juu yenu, na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake.
Sayyid Mojtaba Husayni Khamenei
21 Esfand 1404
Sawa na
22 Ramadhani 1447 Hijria.