
Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa Jumapili, tarehe 8 Machi 2026, Baraza hilo lilitoa rambirambi kufuatia kuuawa shahidi Imam Khamenei pamoja na mashahidi wengine waliouawa katika shambulizi la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 28 Februari. Aidha baraza hilo limelaani vikali uchokozi wa kikatili wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mara tu baada ya shahada ya Imam Khamenei, licha ya kuwepo kwa hali ya vita na vitisho vya moja kwa moja kutoka kwa maadui, Baraza la Wanazuoni Wataalamu halikupoteza muda katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, bali lilianza mara moja mchakato wa kumchagua na kumtangaza Kiongozi mpya.
Iliongeza kuwa baada ya uchunguzi makini na tathmini pana, na kwa kuzingatia wajibu wake wa kidini, Baraza hilo katika kikao chake cha Jumapili lilimchagua na kumtangaza Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuwa Kiongozi wa tatu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel walianzisha mashambulizi dhidi ya Iran kuanzia asubuhi ya Jumamosi, tarehe 28 Februari.
Kwa kujibu uchokozi huo wa Marekani na Israel uliosababisha shahada ya Imam Sayyid Ali Khamenei, pamoja na makamanda kadhaa waandamizi wa kijeshi na mamia ya raia, wakiwemo watoto, Iran ilianzisha Operesheni Ahadi ya Kweli 4, ikitekeleza mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya malengo ya Israel na kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.
Ifuatayo ni taarifa kamili ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu kuhusu kuchaguliwa Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kama Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Enyi taifa tukufu na huru la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amani na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu.
Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, huku likitoa mkono wa pole kufuatia kuuawa shahidi kiongozi mtukufu na mashuhuri, Ayatullah al-Udhma Imam Khamenei (Quddisa Sirruhu), pamoja na mashahidi wengine wa thamani kubwa , hususan makamanda mashujaa na waliojitolea wa vikosi vya ulinzi vya taifa, na wanafunzi wa Shule ya Shajarat Tayyiba katika wilaya ya Minab , na huku likilaani kwa nguvu zote uvamizi wa kinyama wa Marekani mhalifu pamoja na utawala mwovu wa Kizayuni, linapenda kuuarifu umma kwamba Baraza hili mara tu baada ya kusambaa kwa habari ya kuuawa shahidi na kupaa kwake kwa daraja la juu la kiroho la Kiongozi mwenye hekima na busara wa Mapinduzi ya Kiislamu, licha ya hali ngumu ya vita na vitisho vya moja kwa moja kutoka kwa maadui dhidi ya taasisi hii ya wananchi, na pia licha ya mashambulizi ya mabomu dhidi ya ofisi za sekretarieti ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi yaliyosababisha kuuawa shahidi baadhi ya wafanyakazi na walinzi wa taasisi hii, halikusita hata kwa muda mfupi katika mchakato wa kumchagua na kumtangaza Kiongozi wa mfumo wa Kiislamu.
Kwa kuzingatia majukumu yaliyowekwa katika Katiba na kanuni za ndani za Baraza la Wataalamu, hatua na maandalizi muhimu yalichukuliwa mara moja kwa ajili ya kuitisha kikao cha dharura na kumtangaza Kiongozi mpya. Hivyo basi, mipango na uratibu ulifanyika ili kuwawezesha wajumbe waheshimiwa wa Baraza hili walioko katika maeneo mbalimbali ya nchi kukutana, ili, pamoja na uwepo wa utaratibu uliotajwa kwa hekima katika Ibara ya 111 ya Katiba kuhusu kuundwa kwa Baraza la muda, taifa lisikose uongozi.
Baraza la Wataalamu wa Uongozi, huku likithamini na kuheshimu nafasi tukufu ya Wilayat al‑Faqih (Faqihi Mtawala) katika zama za ghaiba ya Imamu wa Zama, Hadhrat Waliy al‑‘Asr (Allah aharakishe kudhihiri kwake), na kwa kuzingatia umuhimu mkubwa wa suala la uongozi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, linatukuza na kuthamini miaka 47 ya uongozi wa hekima uliojengwa juu ya misingi ya heshima, uhuru na mamlaka ya Kiislamu uliotekelezwa na viongozi wawili waliotangulia wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Sambamba na kuhuisha kumbukumbu ya viongozi hao wa kimungu na wa watu, Baraza hili linatangaza kuwa baada ya uchunguzi makini na wa kina, na kwa kutumia uwezo uliopo katika Ibara ya 108 ya Katiba, na kwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria na wa kidini huku likiwa na yakini ya kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, katika kikao chake cha dharura cha leo limemteua na kumtangaza Ayatullah Sayyid Mojtaba Hosseini Khamenei (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwa kura nyingi za wawakilishi waheshimiwa wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi kuwa Kiongozi wa tatu wa Mfumo Mtukufu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mwisho, Baraza hili linatoa shukrani kwa wajumbe wa Baraza la Muda lililoainishwa katika Ibara ya 111 ya Katiba, na linawaalika wananchi wote tukufu wa Iran , hususan wasomi na wahadhiri wa vyuo vya kidini (hawza) na vyuo vikuu , kufanya bay‘a kwa Kiongozi na kudumisha umoja na mshikamano chini ya mhimili wa uongozi wa Kiislamu.
Aidha baraza linamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu kuendelea kunemeesha na kulinda nchi hii na watu wake wakubwa.
Wasalam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Baraza la Wataalamu wa Uongozi
8 Machi 2026
4339300/