Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, Katika taarifa yake Amnesty imesema, shirika hilo lina kumbukumbu za kuuawa Waislamu wasiopungua 200 na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka eneo la magharibi mwa nchi hiyo. Shirika hilo la kutetea haki za binadamu aidha limesema, jamii nzima ya Waislamu imelazimika kukimbia na maelfu ya raia wafuasi wa dini hiyo ambao hawajaweza kukimbia wameuawa na kundi la Anti Balaka la Kikristo na kwamba Wakristo wanawachukulia Waislamu kuwa ni wageni na wanapaswa kuondoka nchini humo lengo ambalo linatimia.
Hayo yamejiri huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akitahadharisha kuwa nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati iko kwenye hatari ya kugawanyika na kusema kuwa anapaswa kufanya jitihada za kuzuia ukatili, kuwalinda raia na kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Nalo Shirika la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch limetaka hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuzuia mauaji ya halaiki ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mkuu wa masuala ya dharura katika shirika hilo Peter Bouckaert amesema Waislamu wanakabiliwa na mustakabali mgumu sana katika nchi hiyo ya kati mwa Afrika na hivyo kuna haja ya hatua za dharura kuchukuliwa ili kuzuia hali ya mambo kuwa mbaya zaidi. Waislamu ni takribani asilimia 15 ya watu milioni 4.6 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ripoti zinasema kuwa magenge ya Wakristo wenye misimamo mikali wamewaua maelfu ya Waislamu nchini humo huku mamia ya maelfu wakilazimika kukimbilia katika nchi jirani. Bouckaert ametoa wito wa kutumwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, 'la sivyo Waislamu hawatakuwa na mustakabali katika nchi hiyo.' Afisa huyo amenukuliwa akisema kuwa Waislamu wametimuliwa kikamilifu katika baadhi ya mitaa katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui.
Amesema kuna njama makusudi za kuhakikisha hakuna Mwislamu anayebakia mjini humo. Aidha amesema misikiti imebomolewa na kwamba ameona msikiti moja tu katika mtaa ambao ulikuwa na misikiti nane mjini Bangui. Kuna askari 1,600 wa Ufaransa na maelfu ya askari wengine wa kulinda amani kutoka nchi za Kiafrika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini wameshindwa kuzuia mauaji ya Waislamu yanayofanywa na magenge ya Wakristo.
1374534