IQNA

Kuzusha mizozo baina ya Waislamu ni kukufuru neema za Allah

23:38 - April 20, 2014
Habari ID: 1397724
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuuletea madhara mshikamano na kuzusha mizozo baina ya Waislamu wa Kishia na Kisunni ni moja ya vithibitisho vya kukufuru neema za Mwenyezi Mungu.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumapili katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra SA binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW mbele ya wasoma kasida na mashairi ya Ahlul Bayt AS hapa mjini Tehran siku ambayo inahesabiwa pia kuwa ni siku ya mama hapa nchini Iran. Ameongeza kuwa: Si sahihi hata kidogo kueneza chuki za kimadhehebu kwani ni jambo lililo wazi kabisa kwamba kueneza mizozo na mifarakano kati ya Waislamu ni sawa na kuwapa upanga maadui wa Uislamu ili wafanikishe uadui wao dhidi ya Uislamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amezungumzia njama za maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu za kujaribu kuharibu imani na itikadi za kidini za wananchi wa Iran na kujaribu kuingiza upotofu katika njia ya harakati ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na harakati ya taifa lenye fakhari nyingi la Iran kwa kutumia vyombo tata vya mawasiliano na kielektroniki. Amesema, lengo la adui ni kutaka kuupigisha magoti Uislamu lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina njia nyingi za kuweza kuvunja na kufelisha njama hizo za maadui ikiwemo mikusanyiko ya kidini kama ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra SA.

1397507

captcha