IQNA

Waziri Mkuu wa kwanza Mwislamu Jamhuri ya Afrika ya Kati

17:42 - August 12, 2014
Habari ID: 1438785
Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bi. Catherine Samba Panza, amemteua Mohammad Kamoun kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo.

Uteuzi huo umechukuliwa katika kalibu ya kuwa na serikali yenye kushirikisha makundi yote ya kisiasa na kidini itakayokubalika na wananchi wote. Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Mohammad Kamoun ambaye ni Mwislamu alikuwa mshauri wa Rais Samba Panza na huko nyuma pia aliwahi kuwa Mkuu wa Hazina katika kipindi cha uongozi wa rais aliyepinduliwa, Francois Bozize.
Uteuzi wa Kamoun unajiri majuma mawili tangu kusainiwa makubaliano ya usitishwaji vita kati ya makundi hasimu ya waasi ya Anti Balaka na Seleka huko Brazzaville, mji mkuu wa Kongo. Kuteuliwa mwanasiasa Mwislamu kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kumeibua hisia mseto na radiamali kutoka kwa watu na makundi mbalimbali ya nchi hiyo. Suala hilo limehuisha kumbukumbu ya mwezi Machi mwaka 2013 wakati Michel Djotodia, kiongozi wa kundi la Seleka alipojitangaza kuwa rais baada ya kumpindua Francois Bozize. Kuingia madarakani Bw. Djotodia ambaye ni Mwislamu kulitumiwa vibaya na baadhi ya wapinzani wake ambao walianzisha fitina za kidini na kusababisha nchi hiyo kutumbukia kwenye vita vya ndani vya kidini kati ya serikali ya Djotodia na wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka. Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya Waislamu kuuawa huku mamia ya maelfu ya wengine wakilazimika kuikimbia nchi kutokana na ghasia hizo. Huku akiwa chini ya mashinikizo ya nchi za Magharibi na baadhi ya nchi jirani, Michel Djotodia alilazimika kuachia ngazi mwezi Januari mwaka huu kwenye kikao maalum cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Katikati mwa Afrika (ECCAS) uliofanyika mjini N'Djamena, Chad.
Kuingia madarakani shaksia wa Kikristo, Catherine Samba Panza, kulitarajiwa kwamba kungepunguza migogoro ya ndani na kurudisha uthabiti wa kisiasa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hata hivyo, mambo yalizidi kwenda kombo chini ya uongozi wake na dunia ikashuhudia machafuko na mgogoro wa kihistoria ambapo Wakristo wa Anti-Balaka walishika silaha na kuanzisha mauaji ya kinyama dhidi ya Waislamu katika kile kilichotajwa kuwa ni ulipizaji kisasi dhidi ya eti jinai za Seleka walipokuwa madarakani. Mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliushtua ulimwengu kiasi kwamba taasisi za kimataifa za kutetea haki za binadamu zilipiga kelele na kulaani mauaji hayo sambamba na kutaka watenda jinai hizo wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Wachambuzi wa siasa za Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaitakidi kuwa, kuweko viongozi wakuu wawili ndani ya serikali ya nchi hiyo yaani Rais Samba Panza ambaye ni Mkristo na Waziri Mkuu mpya, Mahamat Kamoun, ambaye ni Muislamu kunaweza kuleta aina fulani ya uwiano na maridhiano na yumkini hali hiyo ikawa chachu ya kukomeshwa kabisa ghasia na rangaito huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Weledi wa mambo wanasema changamoto kuu inayomkabili Waziri Mkuu mpya ni jinsi ya kuyashirikisha makundi yote hasimu kwenye baraza lake jipya la mawaziri ili serikali itakayoundwa iwe na sura kamili ya kitaifa na itakayokubalika na kila upande.

1438435

captcha