Viongozi wa Kiislamu wanasema Waislamu wanahisi wanabaguliwa kwa jina la 'Mapambano Dhidi ya Ugaidi'. Wabunge nchini Kenya pia wameikosoa serikali kwa kufunga misikiti na kusema kunapaswa kutumiwa njia mbadala kukabiliana na ukosefu wa usalama nchini humo.
Ikumbukwe kuwa wiki iliyopita Polisi nchini Kenya walifunga misikiti mingine miwili katika Kaunti ya Mombasa kutokana na kile walichosema ni maeneo hayo ya ibada kutumiwa kwa ajili ya kueneza misimamo mikali ya kidini na vitendo vya ugaidi.
Katika oparehseni iliyotekelezwa mapema Jumatano, polisi waliingia katika misikiti miwili ya Minaa na Swafaa iliyo katika eneo la Kisauni na kuwatia mbaroni watu 109. Siku ya Jumatatu vijana kutoka misikiti hiyo waliwadunga visu kiholelea raia katika mtaa wa Mlaleo eneo la Kisauni ambapo watu wanne waliuawa. Mauaji hayo yalioonekana ni ya kulipiza kisasi kwani yalifanyika siku moja baada ya polisi kuvamia misikiti miwili ya Musa na Sakina huko huko Mombasa na kuwatia mbaroni vijana 251 huku mmoja wao akiuawa. Aidha maafisa wa usalama wanasema walipata silaha kadhaa katika misikiti hiyo ambayo sasa imefungwa.
Katika oparesheni ya Jumatano maafisa wa polisi wanasema wamepata guruneti moja, bomu tisa za petroli, risasi kadhaa, mapanga pamoja na maandishi yenye kuhimiza ugaidi…/mh