Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imefafanua kuwa katika kipindi hiki cha hali ya mivutano inayochochewa na wale wanaotaka kupindisha mafunzo ya dini na kuchochea migawanyiko, vijana hao watatu waliwakilisha thamani bora za uraia wa ulimwengu mzima na kuonyesha harakati hai za upendo wa kujenga dunia bora kwa ajili ya wote. Matamshi hayo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Matiafa yanakuja baada ya Waislamu kulalamikia vikali kimya cha jamii ya kimataifa kufuatia hujuma ya kigaidi dhidi ya wanachuo hao Waislamu nchini Marekani. Naye Rais Barack Obama wa Marekani hatimaye amevunja kimya kupitia taarifa iliyotolelwa kwa niaba yake, ambapo amesema Polisi ya Upelelezi ya nchi hiyo FBI imeanza uchunguzi kuhusu mauaji ya vijana hao watatu wa Kiislamu. Pia ametoa mkono wa pole kwa familia za marehemu. Deah Shaddy Barakat aliyekuwa na umri wa miaka 23, mke wake Yusor Mohammad Abu-Salha aliyekuwa na miaka 21 na dada yake Razan Mohammad Abu-Salha aliyekuwa na miaka 19 waliuliwa kwa kupigwa risasi siku ya Jumanne iliyopita na mtu aitwaye Craig Stephen Hicks. Muuaji huyo amekuwa akiandika mara kwa mara katika ukurasa wake wa Facebook maelezo ya chuki na uadui dhidi ya Uislamu na Waislamu…/mh