IQNA

Rais wa Iran alaani kuuliwa vijana watatu Waislamu nchini Marekani

16:13 - February 16, 2015
Habari ID: 2858484
Kuuliwa vijana watatu wanachuo Waislamu katika jimbo la Carolina Kaskazini nchini Marekani ni kitendo kinachopaswa kulaaniwa na ni kiashiria kingine cha hatari kubwa ya kuenea kwa vitendo vya ukatili na uchupaji mipaka.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana alituma ujumbe na kulaani kuuliwa vijana watatu wanachuo wa Kiislamu katika jimbo moja nchini Marekani na kueleza masikitiko yake na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa jinai hiyo, jamii ya Waislamu wa Marekani na wapigania uhuru wote na watetezi wa haki za kibinadamu. Rais wa Iran amesema kuwa inatarajiwa kuwa viongozi husika watafanya juhudi zote za lazima kwa ajili ya kulinda haki za raia wote ikiwemo za Waislamu.
Sehemu moja ya ujumbe wa Rais wa Iran inasema kuwa: Ni jambo lenye kutia wasiwasi mno kutokana na ripoti za awali kuonyesha kwamba sababu ya jinai hiyo ni chuki dhidi ya dini na uadui dhidi ya Uislamu; lakini ukweli ni kwamba wale wanaopanda mbegu za chuki dhidi ya dini na hofu juu ya Uislamu, kwa kutaka au kutokutaka wanaeneza vitendo vya ukatili katika jamii.
Jinai hiyo imetokea huku vyombo vya habari vya Magharibi vikiendelea kuonyesha mshikamano wao kwa wahanga wa jarida la kila wiki la Charlie Hebdo la nchini Ufaransa, hata hivyo hatua hizo za kulaani hazijaweza kufichua ukweli wa mambo; ukweli ambao utaonyesha ni nini hasa chanzo na chimbuko la vitendo hivyo vya ukatili na uchupaji mipaka; na ni fikra gani zilizoko nyuma ya pazia na zinazoongoza harakati ya hofu na chuki dhidi ya Uislamu?
Baada ya tukio la kushambuliwa ofisi ya jarida la Charlie Hebdo ambalo liliumiza hisia za Waislamu kwa kuchapisha vibonzo vinavyomdhalilisha Mtume Mtukufu (saw); vyombo vya habari vya Magharibi  vilielekeza mashambulizi yake kwa Uislamu na Waislamu na kulitaja tukio hilo kuwa ni nembo ya fikra za Waislamu; bila hata ya kuashiria chimbuko la vitendo vya kufurutu ada vilivyosababisha kuenea kwa itikadi za Kidaesh na al Qaida. Amma haukupita muda ambapo ni hivi majuzi tu raia mmoja wa Marekani amewauwa wanachuo watatu Waislamu nchini humo, huku duru za habari za Magharibi na za ndani ya Marekani zikiifumbia jicho jinai hiyo kwa kutotoa radiamali yoyote ya maana. Hata hivyo huwenda katika jami iliyojaa misuguano ya Magharibi, matukio mengi kama haya yakafutika haraka katika fikra za waliowengi, lakini yakiendelea kubaki katika historia. Marwa el Sherbini, mwanamke wa Kiislamu aliyekuwa akivaa vazi la stara la hijabu raia wa Misri ni mmoja wa wahanga hawa ambaye tarehe 8 mwezi Julai mwaka 2008 aliuliwa  kwa kucharangwa visu mara 18 na mwanaume mmoja Mjerumani katika mahakama moja nchini Ujerumani huku mumewe na mwanae wakishuhudia hayo kwa macho yao. Bi Sherbini alikuwemo ndani ya mahakama hiyo kama mlalamikaji ili kuwasilisha mashtaka yake dhidi ya mwanaume huyo Mjerumani kwa kosa la kumshambulia na kumdhalilisha. Muuaji huyo wa Kijerumani awali alikuwa amemuita gaidi bi Marwa Sherbini katika bustani moja nchini humo na kisha akamshambulia na kumvua hijabu yake kichwani. Mwanaume huyo Mjerumani alihukumiwa na mahakama moja ya mwanzo ya Ujerumani kulipa faini ya yuro 750, hata hivyo mtuhumiwa huyo alimuuwa mwanamke huyo Mmisri aliyekuwa mjamzito kwa kumcharanga kisu mara 18, wakati wa kusikilizwa kesi iliyokuwa ikimkabili. Kifo cha mwanamke huyo wa Kiislamu kiliacha athari nyingi katika fikra za waliowengi na kuibua maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi na chuki dhidi ya dini Tukufu ya Uislamu. Tab’an radiamali iliyoonyeshwa na vyombo vya habari vya Magharibi ilikabiliwa na ukosoaji mkubwa wa fikra za waliowengi duniani. Vyombo vya habari vya Magharibi viliakisi kwa upana zaidi tukio la kushambuliwa ofisi ya jarida la Charlie Hebdo ikilinganishwa na namna vilivyoitangaza habari ya kuuliwa vijana watatu wa Kiislamu wanachuo huko Marekani. Wakuu wa nchi nyingi duniani hasa wa Magharibi walilaani tukio la kushambuliwa ofisi ya gazeti la Charlie Hebdo nchini Ufaransa, lakini hakuna yeyote kati yao aliyeashiria na kulaani jinai ya Chapel Hill. Moja ya nukta muhimu ilikuwa hii kwamba, viongozi wengi wa nchi za Magharibi na nyengine za kigeni ambao walionekana katika safu ya kwanza ya maandamano ya kuonyesha mshikamano na wahanga wa mashambulizi ya Paris, wenyewe ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa na waasisi wa ugaidi. Kioja ni kwamba hata Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala mtenda jinai wa Kizayuni vile vile alikuwa katika safu ya mbele ya viongozi walioandamana huko Paris.
Ni kwa kuzingatia undumakuwili huo wote na uhakika huu mchungu ndipo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akaandika katika ujumbe wake kwamba: Inatarajiwa kuwa viongozi watafanya jitihada zote za lazima kwa ajili ya kulinda haki za raia wote wakiwemo Waislamu, na akaongeza kwa kueleza kwamba: Wakati umefika sasa wa kuanzisha harakati ya ulimwengu mzima kwa ajili ya kupambana na utumiaji mabavu na vyanzo vya kiutamaduni vya uenezaji chuki dhidi ya dini na uhalifu unaotendwa kutokana na chuki kwa kuwashirikisha wanafikra wote, wasanii, maulamaa wa kidini, jumuiya za kiraia na serikali, ili kuivua jamii ya kimataifa na aibu hii katika karne ya ishirini na moja.

2853973

captcha