IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mazungumzo ya Iran,5+1 ni ya nyuklia tu/ Saudia kuhasirika Yemen

10:41 - April 10, 2015
Habari ID: 3116071
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa hajachukua hatua yoyote kuhusiana na maelewano ya mazungumzo ya nyuklia kati ya taifa hili na kundi la 5+1 kwa kuwa hadi sasa haijafika wakati wa kutoa maamuzi hasa kwa kutilia maanani kwamba bado viongozi wa serikali wamesema kuwa, bado makubaliano hasa hayajafikiwa.

Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo leo Alhamisi mjini Tehran alipokutana na wanawake, malenga na wasomaji kasida za kuwasifu Ahlul Bayt wa Mtukufu Mtume (saw), ambapo sanjari na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa kuwadia maadhimisho ya kuzaliwa Bibi Fatwimat Zahraa (as), binti wa Nabii huyo wa rehma amesema kuwa hajachukua hatua yoyote kwa kuwa viongozi wa serikali wanasema kuwa hadi sasa bado hakujafikiwa makubaliano kamili kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya taifa hili. Amesema kuwa, kile kilichofikiwa katika maelewano hayo bado hakidhamini makubaliano, mwisho wa makubaliano wala muhtawa wa makubaliano yenyewe, kama vile ambavyo hakidhamini pia kwamba mazungumzo hayo yataweza kufikiwa makubaliano ya mwisho, hivyo kutoa pongezi juu ya kadhia hiyo ni suala lisilo na maana. Kiongozi Muadhamu amesema kama ninavyonukuu: "Mimi ninaunga mkono makubalino ambayo yatadhamini izza na utukufu wa taifa la Iran kwa asilimia 100 na ikiwa kuna mtu atakayesema kuwa ninapinga suala la kufikiwa makubaliano, basi atakuwa amesema kinyume na ukweli." Mwisho wa kunukuu. Ayatullahil-Udhma Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa, ikiwa kadhia ya kuondolewa vikwazo itahusisha na suala jengine jipya, huko kufanya mazungumzo yenyewe kutakuwa hakuna maana kwa sababu lengo la kufanyika mazungumzo ni kuondolewa vikwazo, na vikwazo vyenyewe vitapasa viondolewe kikamilifu siku hiyo ya kutiwa saini makubaliano. Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hali ya mambo nchini Yemen na kusisitiza kuwa, watawala wa Saudi Arabia, wamefanya ghalati na makosa kwa kuivamia Yemen na kuanzisha mwenendo mbaya katika eneo. Amesema, mashambulizi dhidi ya taifa na watu wa Yemen ni jinai na mauaji ya umati yanayoweza kufuatiliwa kimataifa. Ameongeza kuwa, kuwaua watoto, kubomoa nyumba, kuangamiza miundombinu na utajiri wa taifa jingine, ni jinai kubwa. Amesisitiza kuwa, bila shaka yoyote, Saudia itakhasirika na kupata hasara katika mashambulizi yake hayo na kamwe haitaweza kushinda.../mh

3112981

captcha