IQNA

Filamu ya Muhammad SAW imewavutia hata wasiokuwa Waislamu Canada

12:13 - September 03, 2015
Habari ID: 3357607
Idadi kubwa ya Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu nchini Canada wameendelea kuvutiwa sana na filamu ya Mtume Muhammad SAW iliyotengenezwa nchini Iran.

Filamu hiyo ambayo imetengenezwa na mtengeneza filamu mashuhuri wa Iran, Majid Majidi na kuonyeshwa kimataifa kwa mara ya kwanza katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Montreal nchini Canada sambamba na kuonyeshwa nchini Iran, imezidi kuwavutia watu wa matabaka mbalimbali wakiwamo Waislamu na wasio Waislamu.
Taarifa zinaeleza kuwa, watu wengi wamekuwa na hamu kubwa ya kutaka kuiona filamu hiyo kiasi kwamba, siku chache kabla ya kuonyeshwa kwake, tiketi za kuingia eneo la maonyesho, zilimalizika haraka.
Imedokezwa kuwa wengi kati ya waliovutiwa zaidi na filamu hiyo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad SAW, ni wafuasi wa dini nyingine.
Idara ya Sinema nchini Canada umeripoti kwamba imepokea maombi zaidi ya kuongezwa maradufu tiketi na maeneo ya kuonyeshea filamu hiyo ya Muhammad SAW nchini humo.

Filamu ya Mtume Muhammad SAW iliyozinduliwa Alkhamisi iliyopita inaendelea kuonyeshwa katika kumbi 150 za sinema hapa nchini Iran. Filamu hiyo inasimulia kisa cha Mtume Muhammad SAW kabla ya kuzaliwa mtukufu huyo na kipindi cha utotoni mwake.
Filamu hiyo yenye dakika 171 imetengenezwa kwa bajeti ya dola milioni 50 na imetajwa kuwa filamu iliyogharimu kiasi kikubwa zaidi cha fedha nchini Iran na utengenezaji wake umechukua kipindi cha miaka mitano.
Wiki hii Filamu hiyo imeendelea kuwavutia watazamaji wa filamu katika kumbi za sinema kote katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Imearifiwa kuwa katika siku saba za kwanza mauzo ya tiketi za filamu hiyo yemefika takribani nusu milioni dola nchini.../mh

3355996

captcha