Akiashiria matamshi ya viongozi wa Marekani ya kulinda fremu ya vikwazo, Kiongozi Muadhamu amesema, "Kama taifa la Iran lililegeza kamba katika baadhi ya mambo kwenye mazungumzo hayo, lengo la kufanya hivyo lilikuwa ni kuondolewa vikwazo; kwani kinyume na hivyo Iran ilikuwa inaweza kutengeneza mashinepewa na kufikisha elfu 50 mpaka elfu 60 kwa kipindi cha muda mfupi tu badala ya mashinepewa elfu 19 ilizonazo sasa na kuendelea kurutubisha madini ya urani kwa asilimia 20."
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo mjini Tehran alipokutana na mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu linalomchagua Kiongozi Muadhamu na kusimamia kazi zake.
Kiongozi Muadhamu aidha amesisitiza juu ya ulazima wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran (Bunge) kujadili mwafaka wa nyuklia na kubainisha kwamba, hana maelekezo au nasaha zozote kwa Bunge kuhusiana na namna ya kujadili mwafaka huo, kuupasisha au kuupinga.
Kiongozi Muadhamu amebainisha moja ya misdaqi za matarajio ya Wamarekani na kusema kuwa, miongoni mwa siasa za Marekani Mashariki ya Kati ni kuuangamiza muqawama kikamilifu, kuidhibiti kikamilifu Syria na Iraq na kwamba, wana matarajio ya kuiona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikifuata mkondo huo; lakini katu jambo hilo halitatokea. Ayatullah Khamenei amekumbusha nukta muhimu kuhusiana na propaganda za kambi ya ubeberu za kuwatwisha maneno bandia viongozi na watu wenye maamuzi katika nchi mbalimbali na kusema kuwa, katika fasihi ya mfumo wa kibeberu maneno kama ugaidi na haki za binadamu yana maana na fasili maalumu. Amesema, katika fasihi yao mashambulio mtawalia ya miezi sita dhidi ya wananchi wa Yemen na kuuawa wananchi wasio na hatia wa Gaza sio ugaidi, na hata ukandamizaji unaofanywa dhidi ya wananchi wa Bahrain hauhesabiwi kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, katika mfumo wa fasihi wa ubeberu, mapambano ya kujitetea huko Lebanon na Palestina yanahesabiwa kuwa ni ugaidi.
Iran na nchi za 5+1 yaani China, Russia, Marekani, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zilifikia muafaka mjini Vienna kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran.
Kwa mujibu wa mapatano hayo Iran itapunguza baadhi ya shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani mkabala wa kuondolewa vikwazo vyote ilivyokuwa imewekewa.../mh