Kiongozi Muadhamu ametoa kauli hiyo Jumamosi jioni hapa mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Kyrgyzstan Almazbek Atambayev. Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Rouhani wa Iran, Ayatullah Khamenei ameashiria matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Kyrgyzstan kuhusu nia ya nchi yake ya kuzuia jeshi la Marekani kutumia kituo cha jeshi la anga cha Manas nchini humo na kusisitizia haja ya kukabiliana na tabia za kibeberu za madola makubwa duniani. "Madola makubwa ya kibeberu na vamizi daima huwa yanapanga njama dhidi ya nchi zote duniani; lakini Uislamu unataka heshima ya mataifa ya Waislamu; na njia pekee ya kukabiliana na shari ya madola hayo makubwa ni mapambano na kuimarisha uhusiano baina ya nchi za Waislamu," amesema Ayatullah Khamenei. Kiongozi Muadhamu amesema, msingi wa sera za kigeni za Iran ni kuimarisha uhusiano kati ya nchi za Kiislamu. Kwa upande wake, Rais Atambayev wa Kyrgyzstan amebainisha furaha yake kwa kuitembelea Iran na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu na Kyrgyzstan ni nchi mbili zenye uhusiano wa kidugu, dini, historia na utamaduni wa pamoja. Ameongeza kuwa, moyo wa kutaka uhuru na kujitegemea uko hai katika mataifa haya mawili.../mh