Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran Alhamisi imeripoti kuwa, baada ya kupita muda wa wiki mbili tangu kutokea maafa ya Mina na kuuwa maelfu ya Mahujaji, Bandar bin Mohammad Hajjar, Waziri wa Masuala ya Hija wa Saudia amemtumia ujumbe Saeed Ohadi, Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran na kutoa mkono wa pole kwa ulimwengu wa Kiislamu na hususan taifa la Iran kutokana na maafa ya Mina. Katika ujumbe huo wa rambirambi, Waziri wa Hija wa Saudi Arabia pia amesisitiza kuwa: Orodha ya majina na maelezo ya hati za mahujaji wa Kiirani walioaga dunia itakabidhiwa kwa Wizara ya Hija ya Saudia ili ikamilishe masuala yanayohitajika na hivyo kuweza kuisafirisha hadi Tehran miili ya Mahujaji wa Iran waliopoteza maisha huko Mina.
Maelfu ya Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu wakiwemo Mahujaji 465 wa Iran walipoteza maisha sambamba na Siku kuu ya Idul Adh'ha wakati walipokuwa wakitekeleza moja ya amali muhimu za ibada ya Hija huko Mina kutokana na kutowajibika watawala na maafisa husika wa Saudia.