Mapema siku ya Jumamosi, makundi ya Mahujaji walielekea katika eneo la Jamarat huko Mina, ambako walishiriki katika ibada ya kutupa mawe. Ibada hii, inayojumuisha kutupa kokoto kwenye nguzo tatu za mawe, ni alama ya kujitenga na shari ya shetani na ni miongoni mwa ibada kuu za Hija.
Mamlaka za Saudi Arabia, zikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani, zilitoa miongozo kwa Mahujaji kuhusu kufuata njia maalum na ratiba ili kudhibiti umati wa watu na kuhakikisha usalama wakati wa ibada hiyo. Vikosi vya usalama na huduma za afya vilitawanywa Mina na Makkah ili kutoa msaada kwa mahujaji waliofika kwa wingi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mamlaka Kuu ya Takwimu ya Saudi Arabia, jumla ya Mahujaji 1,673,230 walishiriki katika ibada ya Hija kwa mwaka huu wa Kiislamu 1446 Hijria. Kati yao, 1,506,576 walitoka nje ya Saudia, huku 166,654 wakiwa ni mahujaji wa ndani, raia wa Saudi Arabia na wakazi wa kigeni wanaoishi humo.
Idadi kubwa ya Mahujaji kutoka nje ya nchi ni ushahidi wa juhudi za Saudi Arabia katika kuwezesha Waislamu kutoka duniani kote kutekeleza ibada ya Hija, hasa baada ya vizuizi vilivyotokana na janga la COVID-19.
Ibada ya Hija hufanyika kwa muda wa siku kadhaa na inajumuisha ibada mbalimbali katika miji mitakatifu ya Makkah na maeneo ya jirani. Hii ni pamoja na kusimama katika uwanja wa Arafah, kukaa Muzdalifah usiku, kuwepo Mina, na kuchinja mnyama kwa katika sikukuu ya Idul Adha. Tawafu ya kuaga (Tawafu al-Wada‘), inayohusisha kuzunguka Kaaba mara saba, ndiyo inahitimisha ibada ya Hija.
Hija ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani, na ni nguzo ya tano ya Uislamu. Tukio hili huambatana na maandalizi ya miezi mingi kwa Mahujaji, wengi wao wakitunza fedha kwa miaka ili kuweza kupata fursa hii tukufu.
3493360