IQNA

Kiongozi Muadhamu alaani kuuawa shahidi Sheikh Nimr

13:25 - January 03, 2016
Habari ID: 3470009
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelaani vikali jinai kubwa ya Saudi Arabia ya kumuua shahidi mwanazuoni muumini na madhulumu Sheikh Nimr Baqir al-Nimr.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo asubuhi ya leo katika darsa ya Kharij ya Fikihi (masomo ya juu kabisa ya fikihi) na kusisitiza juu ya ulazima wa ulimwengu kuhisi kuwa na majukumu mkabala na jinai hii na jinai nyingine za Saudi Arabia huku nchini Yemen na Bahrain.

Ayatullah Khamenei amebainisha kwamba, hapana shaka kuwa, athari ya damu iliyomwagwa kidhulma ya shahidi huyu madhulumu itaenea kwa kasi na ulipizaji kisasi wa Mwenyezi Mungu utawakumba wanasiasa wa utawala wa Aal Saud.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, alimu huyo madhulumu hakuwa akiwachochea watu kushika silaha na kukabiliana na utawala wa Saudia na wala hakufanya njama za siri dhidi ya utawala huo, bali alililokuwa akilifanya ni kuukosoa wazi utawala wa Riyadh na kuamrisha mema na kukataza mabaya.

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, hatua ya watawala wa Saudia ya kumwaga kidhulma damu ya shahidi Nimr ni kosa la kisiasa la serikali ya Riyadh ambalo kwa haraka sana balaa lake litawakumba wanasiasa wa utawala huo wa Kifalme.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuteswa na kufanyiwa madhila wananchi wa Bahrain na vikosi vya Saudia, kubomolewa misikiti na nyumba zao na vile vile kushambuliwa kwa mabomu wananchi wa Yemen kwa zaidi ya miezi kumi sasa ni jinai nyingine za utawala wa Saudi Arabia.

3463996

captcha