IQNA

Wanawake Gambia watakiwa kuvaa Hijabu kazini

11:44 - January 08, 2016
Habari ID: 3470023
Serikali ya Gambia imetoa tangazo na kuwataka wanawake walioajiriwa na serikali wametakiwa kuvaa vazi la Hijabu wakiwa kazini.

Kwa mujibu wa tovuti ya Jollof News, hivi karibuni Rais Yahya Jammeh wa Gambia aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kiislamu.Jammeh ambaye aliwahi kuwa afisa wa jeshi na ambaye kawaida hutembea akiwa amebeba Qur'ani na tasbihi mkononi, baada ya kuitangaza nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi kuwa ya Kiislamu alisema: "Uamuzi huu umechukuliwa kwa ajili akthari ya watu wa Gambia ni Waislmau na kuna haja ya kuimarisha utambulisho wa Kiislamu nchini."

Aliongeza kuwa, "Iwapo Wagambia watazingatia mafundisho ya Mwenyezi Mungu, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Gambia itastawi katika nyanja zote za kibinadamu na kiuchumi."Ingawa rais wa Gambia aliwahi kusema kuwa hakutakuwa na vizingiti vya mavazi na kwamba wafuasi wa dini nyinginezo wataheshimiwa, idara ya usimamizi wa wafanyakazi wa serikali amewataka wakuu wa mashirika na taasisi zote za kiserikali kuhakikisha kuwa wanawake wote wanavaa Hijabu kazini. Rais Jammeh anakosolewa kwa kuamuru wanawake wavae Hijabu kazini katika hali ambayo mke wake binafsi huonekana hadharani pasina kuvaa Hijabu.

Rais Jammeh ambaye mwaka 2013 alitangaza kujitoa nchi hiyo katika Jumuiya ya Madola, Commonwealth na kuitaja kuwa ni ukoloni mamboleo, anataraji nchi za Kiarabu zitaisaidia nchi yake ili iweze kuziba pengo la misaada iliyokatwa na itakayokatwa ya madola ya Magharibi. Machi mwaka huu serikali ya Gambia ilibadilisha lugha yake rasmi ya Kiingereza na kuifanya kuwa Kiarabu.

Gambia ina wakazi milioni moja na laki nane huku asilimia 95 wakiwa ni Waislamu. Gambia ilikoloniwa na Uingereza hadi mwaka 1965 ilipopata uhuru.

Nchi hiyo inategemea zaidi kilimo na utalii kama sekta kuu na uti wa mgongo wa uchumi wake.

http://iqna.ir/fa/news/3464982

captcha