IQNA

Rais wa Iran akataa kushiriki karamu yenye pombe Ufaransa

19:01 - January 28, 2016
Habari ID: 3470095
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekataa kushiriki kwenye karamu ya chakula cha mchana iliyotayarishwa na mwenyeji wake wa Ufaransa, François Hollande baada ya ikulu ya Elysée kushikilia msimamo wake wa kuwepo pombe katika meza ya chakula iliyotayarishwa kwa heshima ya Rais wa Iran.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti kuwa, msimamo huo umechukuliwa na Rais Rouhani baada ya Ufaransa kusisitiza kwamba mvinyo katika meza ya karamu ya viongozi mbalimbali wa heshima ni sehemu ya utamaduni wa Ufaransa. Badala yake Rais Rouhani hatashiriki katika karamu ya chakula cha mchana iliyotayarishwa na mwenyeji wake wa Ufaransa kutokana na kuwepo pombe na nyama zisizo halali katika meza hiyo.

Kabla ya kuelekea Ufaransa, Rais Rouhani alitembelea Italia ambako alikutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo. Akiwa Italia Rais Rouhani alizungumza na Waziri Mkuu, Matteo Renzi na kutembelea Jumba la Makumbusho la Capitoline katika mji mkuu wa Italia, Roma. Wakati huo masanamu yote uchi ya Jumba la Makumbusho la Capitoline yalifunikwa wakati wa mkutano wa Rais Hassan Rouhani na Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi. Shirika la habari la Italia, ANSA limeripoti kuwa masanamu ya jumba hilo la makumbusho yalifunikwa kwa heshima ya Rais wa Iran aliyeitembelea Italia. Vilevile pombe, mvinyo na vyakula visivyo halali havikuwekwa katika meza ya karamu ya chakula cha usiku iliyotayarishwa na Waziri Mkuu wa Italia kwa ajili ya Rais Hassan Rouhani na ujumbe ulioandamana naye ikiwa ni kuonesha heshima kwa maadili na sheria za Kiislamu.

3470868

captcha