IQNA

Wanawake Mashia na Masuni Marekani washirki mkutano wa pamoja

18:49 - May 01, 2016
Habari ID: 3470282
Wanawake Waisalmu wa madhehebu za Shia na Suni nchini Marekani wamefanya kongamano maalumu kwa lengo la kuimarisha umoja wa Kiislamu baina yao.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, wanawake hao Waislamu katika jimbo la Ohio nchini Marekani wamefanya kongamano maalumu ili mbali na kuzidi kuelewana, kuonesha kuwa masuala yanayowaunganisha pamoja ni mengi zaidi kulinganisha na wanayohitilafiana.

Halikadhalika wanafanya mkakati wa kuungana pamoja kukabiliana na misimamo mikali ya kidini sambamba na kutangaza ujumbe wa amani wa Uislamu.

Golchin Ozer, mtafiti wa taarifa za kitabibu katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Ohio, ambaye aliwakilisha jamii ya Kisuni katika kikao hicho alisema sauti za misimamo mikali zinasikika kila mara katika vyombo vya habari, lakini wanawake Waislamu walioko nchini Marekani wanaishi kwa kufuata msimamo wa wastani.

Ozer ameongeza kuwa Mashia na Masuni wana nukta za pamoja katika mambo mengi kuliko wanayotafautiana na kwamba wanawake Waislamu wanataka kutilia mkazo juu ya nukta hizo za pamoja.

Aysar Hamoudi, tabibu mstaafu wa jamii ya Waislamu wa Kishia kutoka eneo la Dublin-Granville katika mji wa Worthington amesema, akthari ya wanaoathirika na jinai za kundi la kigaidi la ISIS au Daesh ni Waislamu, na kwamba magaidi hao hawana dini yoyote kwa sababu mtu anayemwamini Mungu hawezi kufanya jinai kama hizo. Hamoudi ameongeza kuwa hakuna dini yoyote inayofunza mtu kuchukia ndugu zake, wananchi wenzake na binadamu kwa ujumla; na Uislamu ni dini ya udugu. Amesema idadi kubwa ya jamaa katika familia yake wameuawa katika hujuma za kigaidi za ISIS nchini Iraq.

3459674
captcha