Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuweko mabadilishano ya uzoefu katika nyuga
tofauti za kielimu, kiteknolojia, kisiasa, kijamii na kiusalama ni kwa manufaa
ya nchi zote hizi mbili na kuongeza kuwa: Sisi katika siasa zetu za kigeni
tunapendelea zaidi kuwa na ushirikiano na nchi za Asia kwani tuna mambo mengi
ya pamoja ya kiutamaduni na kihistoria baina yetu na ni kwa sababu hiyo ndio
maana tunaamini kuwa, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kufikiwa maelewano, mwafaka
na ushirikiano baina ya nchi za bara hilo ikiwemo Korea Kusini ambayo ni moja
ya nchi zilizoendelea barani Asia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matatizo muhimu ya
kiusalama yaliyopo katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla na
kusisitiza kwamba: Kama hivi sasa hakutakuwa na mapambano ya kweli dhidi ya
hatari ya ugaidi na usalama, basi kukabiliana na hatari hiyo katika siku za
usoni litakuwa ni jambo zito zaidi na hakuna nchi yoyote itakayobakia salama
mbele ya hatari ya ugaidi.
Vile vile ameashiria namna Wamarekani wanavyougawanya ugaidi makundi mawili
kati ya ugaidi mzuri na ugaidi mbaya na kusema kuwa: Wamarekani wanajinadi kuwa
wanapambana na ugaidi lakini kivitendo hawapambani kwa dhati na ugaidi wakati
ambapo ugaidi wa namna yoyote ile ni hatari kwa usalama wa mataifa yote duniani
na sababu yake ni kuwa iwapo usalama na amani haitkuwepo, maendeleo
yanayotakiwa nayo hayawezi kupatikana.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amezungumzia ushirikiano na maafikiano baina
ya nchi mbili za Iran na Korea Kusini na kugusia pia mambo yanayopasa kupewa
kipaumbele katika ushirikiano wa pande hizo mbili na kusema: Kuna uwezekano
mkubwa wa kuwepo ushirikiano wenye faida kubwa baina ya Iran na Korea Kusini
lakini vipaumbele vyetu katika ushirikiano huo havimalizikii tu katika masuala
ya biashara bali inabidi kutiwe saini mikataba inayohitajiwa na Iran katika
miundombinu na uchumi kwa ujumla.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kuwa, kuathiriwa
maelewano na mikataba ya pande mbili na mambo ya pembeni ni moja ya mambo ya
kimsingi yanayopasa kuwekewa mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa hayatokei
katika ushirikiano wa nchi mbili na kusisitiza kuwa: Si sahihi kuruhusu
uhusiano wa Iran na Korea Kusini uathiriwe na misimamo na ushawishi wa
Marekani, bali inabidi uhusiano wa nchi hizi mbili uwe wa kuendelea, wa kudumu,
usiotetereka, wa kiudugu na wa kupendana kikweli kweli.
Vile vile amegusia historia takriban ndefu - lakini yenye panda shuka na
misukosuko mingi - ya uhusiano wa Iran na Korea Kusini na kusisitiza kuwa: Kwa
bahati nzuri serikali iliyoko madarakani huko Korea Kusini hivi sasa ni
serikali inayopenda maelewano na kwa upande wake, Iran ina nafasi kubwa na
nyingi pamoja na nguvu kazi mahiri ya vijana wenye nguvu, wenye vipaji na
wasomi, suala ambalo linatoa fursa ya kuwepo ushirikiano wa kudumu, mpana na
usioyumba baina ya nchi mbili.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran, Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amesema kuwa ziara yake ya
kutembelea Tehran ni fursa yenye thamani kubwa kwa ajili ya kustawisha uhusiano
wa pande mbili na kuongeza kiwango cha kuaminiana. Ameongeza kuwa: Sisi hata
katika kipindi cha kuwekewa vikwazo Iran tulijitahidi kuendelea kuwepo nchini
Iran kadiri tulivyoweza.
Rais wa Korea Kusini amesema, Iran ni nchi yenye fursa nyingi yenye nguvu kazi
muhimu, madhubuti na yenye taathira kama ambavyo pia Iran ni nchi iliyopo
kwenye eneo la kijiografia lenye umuhimu wa kipekee. Amesema: Ni matumaini yetu
kuwa uhusiano wa nchi hizi mbili hususan katika sekta ya uchumi ya ustawi
utaimarika zaidi.
Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amegusia pia mitazamo ya Kiongozi Muadhamu
wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ustawi wa kiuchumi wa nchini Iran na vile vile
sisitizo lake la mara kwa mara la kutiliwa mkazo ustawi wa kielimu, kiuchumi na
kiviwanda kwa kutegemea nguvu na suhula za ndani ya nchi na kusema: Nina yakini
kwamba sisitizo lako juu ya ustawi na juu ya kuboreshwa uchumi wa Iran
litailetea nchi hii mustakbali mzuri sana, na sisi pia tuko tayari kuongeza
ushirikiano wetu katika nyuga tofauti kama vile mazingira, sayansi na
teknolojia pamoja na masuala ya kiuchumi.
3494315