IQNA

Saudia yawazuia Wairani kutekeleza ibada ya Hija

17:09 - May 29, 2016
Habari ID: 3470344
Saudi Arabia imeweka vizingiti na kuwazuia wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Waziri wa Utamaduni na Muongoza wa Kiislamu Iran, Dkt. Ahmad Jannati akizungumza Jumapili hii amesema Saudia imeweka vizingiti vingi na kutekeleza njama zinginezo haribifu na kwa njia hiyo kuwazuia wananchi wa Iran kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu. Ameongeza kuwa wakuu wa Saudia pia wamekuwa na muamala mbovu na wajumbe wa Iran waliofika nchini humo kwa ajili ya duru mbili za mazungumzo kuhusu Hija. "Kwa mtazamo wangu, Saudia imetekeleza njama za makusudi kuwazuia raia wa Iran kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu."

Shirika la Hija na Ziara za Kidini Iran pia limetoa taarifa na kusema: "Pamoja na kuwepo jitihada za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wakuu wa Saudia wamepuuza haki isiyopingka ya Wairani ya kutekeleza ibada ya Hija."

Siku ya Jumamosi Wizara ya Hija ya Saudi Arabia ilisema imekutana na maafisa wa Hija wa Iran lakini Mkuu wa Shirika la Hija la Iran Saeed Ohadi amesema wakuu wa Riyad walikataa matakwa ya Iran ya kudhaminiwa usalama na heshima ya Mhujaji Wairani.

Kwa muda wa zaidi ya miezi minne iliyopita Iran imekuwa ikifanya juhudi za kufuatilia namna wananchi wake watakavyokwenda kutekeleza amali ya Hija mwaka huu, lakini viongozi wa Saudia wanaendelea kukataa mapendekezo ya Iran katika masuala kama vile viza, usafiri wa anga na kudhaminiwa usalama wa mahujaji wa Iran, hasa kutokana na kuwa miezi kadhaa iliyopita Saudia ilifunga ubalozi wake nchini Iran. Ubalozi wa Uswisi unalinda maslahi ya Saudia nchini Iran lakini wakuu wa Saudia wamekataa mahujaji Wairani wachukue visa kupitia ubalozi huo.

Maafisa wa Taasisi ya Hija ya Iran wanasema kuwa, kwa kuzingatia kwamba, hisa ya Iran ya Hija ni mahujaji 65 elfu na kwa sasa hakuna uhusiano wa kibalozi kati ya Tehran na Riyadh, haitawezekana kwa mahujaji hao kwenda kuchukua viza katika nchi ya tatu. Mbali na hayo, Saudia imetangaza kuwa, hakuna ndege yoyote kutoka Iran yenye haki ya kutua nchini Saudia na kwamba, mahujaji wa Kiirani hawapaswi kushiriki katika marasimu ya kujibari na washirikina katika ibada ya Hija.

Sisitizo la Iran la kulindwa haki, izza na usalama wa mahujaji wake katika ibada ya Hija linatolewa katika hali ambayo, ibada ya Hija mwaka jana iliambatana na matukio machungu ya umwagikaji damu kutokana na usimamizi mbovu wa Wasaudi.

Katika tukio la kwanza la kuanguka winchi ndani ya Masjidul Haram, takribani mahujaji 180 walipoteza maisha wakiwemo mahujaji wa Kiirani. Aidha kulitokea maafa makubwa huko Mina kutokana na uzembe na usimamizi mbovu wa viongozi wa Saudia na hatua yao ya kufunga njia zinazoelekea katika sehemu ya kumpiga mawe shetani. Maelfu ya mahujaji walipoteza maisha wakiwemo mahujaji 465 wa Kiirani.

Ujumbe wa Saudia uliofanya mazungumzo na Iran ulikiri kuwa hauna uwezo wa kuchukua maamuzi kuhusu matakwa ya Iran na kwamba maamuzi yalipaswa kuchukuliwa na maafisa wengine wa ngazi za juu katika utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Saud.

3502085
Kishikizo: hija iran saudia ouhadi iqna
captcha