Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, akizungumza Jumatatu katika mkoa wa Azarbaijan Magharibi, Rais
Rouhani amesema ibada ya Hija na miji mitakatifu ya Makka na Madina ni
ya Waislamu wote na kwamba Ibada ya Hija ni sehemu ya kutekelezwa
matakwa ya Umma wa Kiislamu. Ameongeza kuwa wale wanaodai kuwa eti ni wahudumu wa Misikiti Miwili
Mitakatifu wanatekeleza hatua ya kitoto ya kuzuia Njia ya Mwenyezi Mungu
na Hijja huku wakieneza machafuko katika eneo, na yote hayo ni kwa
maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Siku ya Jumapili Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran
alisema njama na vizingiti vya Saudia ni jambo ambalo limewazuia Wairani
kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu.
Naye Mkuu wa Shirika la Hija na Ziara za Kidini la Iran Saeed Ohadi
amebainisha sababu ambazo zimepelekea Mahujaji Wairani washindwe
kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu. Amebaini kuwa Wasaudi wamepiga
marufuku kuwekwa bendera ya Iran katika majengo ya Mahujaji Wairani.
Aidha wameweka vizingiti kuhusu idadi ya zahanati za Iran katika msimu
wa Hija sambamba na kuzuia madawa yanayotumiwa na Mahujaji Wairani.
Aidha amesema Wasaudi wamekataa ushanga wa mkononi wa kielektroniki
ambao Iran ilikuwa imetengeneza kwa ajili ya kuwatambulisha Mahujaji
wake huku wakisema watatengeneza ushanga ambao watawalazimisha Wairani
kuuvaa. Ohadi amesema Wasaudi pia wamepiga marufuku baadhi ya hafla za
Mahujaji Wairani jambo ambalo Iran haikulikubali. Afisa huyo wa Hija wa
Iran pia amesema Saudi Arabia inawadhalilisha Wairani kisiasa na hata
wakati wa mazungumzo kuhusu Hija Wasaudi walionyesha muamala mbovu sana.
Mkuu wa Shirika la Hija la Iran pia amesema maafisa wa Saudia kwa
kawaida huvunjia heshima nakala za Qur’ani zilizochapishwa nchini Iran
na kuwapokonya Mahujaji Wairani nakala hizo za Qur’ani huku wakizirusha
huku na kule kwa madharau.