IQNA

Matembezi ya Waislamu Tanzania kuwakumbuka mateka wa Karbala+PICHA

20:50 - October 16, 2016
Habari ID: 3470616
Waislamu mjini Dar es Salaam, Tanzania wameshiriki katika matembelezo ya kuwakumbuka mateka wa Karbala na hasa Bibi Zainab SA.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, matembezi hayo ya kufungamana na Ahul Bayat AS na kuwakumbuka wafungwa wa Karbala na hasa Bibi Zainab SA yamefanyika leo Jumapili katika eneo la Temeke jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na IQNA, Mwambata wa Utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania Bwana Ali Baqeri amesema katika hafla hiyo, Maulana Sheikh Hemed Jalala, Mkuu wa Hawza (Chuo Kikuu cha Kidini) ya Imam Sadiq AS ya Dar es Salaam, amehutubu kuhusu falsafa ya Ashura. Matembezi hayo yalikuwa katika njia yenye urefu wa kilomita saba huku washiriki wakitoa nara ya 'Labbayk ya Hussein' sambamba na qasida za kutangaza utiifu wao kwa Harakati ya Imam Hussein AS.

Matembezi hayo pia yalimshirikisha Shehe Mkuu wa Ahul Sunna mjini Dar es Salaam , Sheikh Mussa Salim Al Hadi , ambaye katika hotuba yake amesema, harakati ya Ashura ni bima iliyouhifadhi Uislamu.

Sheikh Al Hadi amesistiza kuhusu kulinda umoja wa Kiislamu na kuongeza kuwa, Imam Hussein AS alikuwa chimbuko la umoja wa Waislamu. Ameongeza kuwa, "daima tunapaswa kukumbuka ujumbe wa Imam Khomeini MA ambaye alisisitiza kuhusu udharura wa umoja wa ulimwengu wa Kiislamu."Matembezi ya Waislamu Tanzania kuwakumbuka mateka wa KarbalaMatembezi ya Waislamu Tanzania kuwakumbuka mateka wa KarbalaMatembezi ya Waislamu Tanzania kuwakumbuka mateka wa Karbala

Mwishoni mwa matembezi hayo ambayo yaliandaliwa na Bilal Muslim Mission ya Tanzania, washiriki walikusanyika katika Kituo cha Bilal Muslim ambapo Sheikh Ali Dina, Imam wa Msikiti wa Jamia wa Khoja Shia Ithnaasheri alisema kuwa Imam Hussein alitoa funzo la kupambana na dhulma na kwamba alisisitiza kuwa 'usidhulumu mtu na wale usikubali kudhulumiwa.'

Bibi Zainab SA alishuhudia tukio chungu, gumu, la kusikitisha na la kihistoria la Karbala. Wakati alipouawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW,  Imam Hussein AS na wafuasi wake 72 katika siku ya Ashura huko Karbala, Bibi Zainab SA alibeba jukumu zito kabisa la tukio hilo. Mbali na hayo alikuwa na jukumu la kuwaongoza manusura wa Ahlul-Bayt wa Mtume SAW ambao walikuwa mateka kutoka mjini Karbala hadi Sham. Kwa hakika Zainab SA alikuwa simba wa kike katika matukio yote ya Karbala tangu mwanzoni mwa mapambano hayo, wakati alipokuwa katikati ya maiti za mashahidi wa haki, pindi alipochukuliwa mateka na utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya hadi alipokuwa katika kasri la mfalme dhalimu Yazid huko Sham.

Bibi Zainab SA alikuwa kigezo bora, hatibu hodari, mwalimu mahiri na mwendelezaji wa harakati adhimu ya mapambano ya Ashura. 

3538177


captcha