IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani haina nia ya kung'oa mzizi wa magaidi wa kitakfiri

6:43 - December 12, 2016
Habari ID: 3470736
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Marekani daima inapinga nguvu na kupata uwezo nchi za Kiislamu ikiwemo Iraq na kamwe hatupaswi kuhadaika na dhahiri na tabasamu za Wamarekani.

Ayatullah Seyyed Ali Khamenei ameyasema hayo Jumapili mjini Tehran katika mazungumzo yake na Ammar al Hakiim, Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Mashia wa Iraq na ujumbe alioandamana nao.

Amesisitiza kuwa, kinyume na madai yao, Wamarekani hawana nia ya kung'oa mzizi wa magaidi wa kitakfiri na wanafanya jitihada za kubakisha baadhi ya magaidi hao kwa ajili ya kuyatumia katika malengo yao ya baadaye.

Ayatullah Khamenei ameashiria jinsi kundi la Daesh au ISIS lilivyokuwa likiuza mafuta ya Iraq na kusema, kipindi hicho Wamarekani waliketi na kutazama tu harakati ya msafara wa magari ya kubeba mafuta ya petroli bila ya kuushambulia; kwa msingi huo haipasi kuwaamini Wamarekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mustakbali wa Iran uko wazi na utakuwa mwema na mzuri kuliko hali ya sasa na kuongeza kuwa: Maendeleo ya Iraq yatakuwa na manufaa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vilevile uratibu na ushirikiano wa pande hizi mbili utakuwa na faida kwa nchi zote mbili.

Ayatullah Khamenei ameeleza kufurahishwa na hatua ya kuundwa muungano wa makundi ya Waislamu wa Kishia nchini Iraq na kulitaja kuwa ni tukio muhimu. Vilevile amesisitiza udharura wa kulindwa nguzo na misingi ya umoja huo. 

Vilevile ameyataja majukumu ya mwenyekiti, wanachama na makundi yote yanayounda Muungano wa Kitaifa wa Mashia wa Iraq kuwa ni mazito sana na kusema kuwa, utendaji wao utakuwa na taathira kwa Iraq, eneo la Mashariki ya Kati na Uislamu.

Ayatullah Khamenei amewashukuru wananchi wote wa Iraq na viongozi wa nchi hiyo kutokana na mapokezi na ukarimu wao mkubwa kwa watu waliokwenda kumzuru Imam Hussein AS katika shughuli ya Arubaini na kusema matembezi ya Arubaini ni tukio adhimu na lisilo na kifani.

Kwa upande wake Sayyid Ammar Hakim, Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Iraq amesifu misaada na himaya ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran na kusema: Miongoni mwa mambo muhimu ya Muungano wa Kitaifa wa Mashia wa Iraq ni kupasishwa sheria ya al Hashdu Shaabi (makundi ya kujitolea ya wananchi) katika Bunge la nchi hiyo.   

3552868/


captcha