Hivi karibuni Rais Trump wa Marekani alisema nchi yake haituanga mkono
suluhisho hilo la nchi mbili. Sayyed Nasrallah amesema hatua hiyo ya
Marekani ni muhimu kwani imehitimisha hadaa ya Israel kwa Wapalestina na
kusema hivi sasa malengo halisi ya utawala wa Tel Aviv yatabainika.
Kuhusu vitisho vya hujuma ya kijeshi dhidi ya Iran, Sayyed Nasrallah
amesema vitisho hivyo ni vita vya kisaikolojia kuishinikiza Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran ilegeze misimamo yake ya msingi. Amesema hivi sasa
Marekani haina uwezo wa kuanzisha vita dhidi ya Iran kwani inafahamu
kuwa Iran haitakuwa peke yake katika vita hivyo.Katika mahojiano maalumu na Kanali ya Kwanza ya Shirika la Utangazaji la Iran IRIB yaliyorushwa hewani Jumatatu usiku, Nasrallah amesisitiza kuwa, Iran inatuma ujumbe mzito wa mshikamano na Palestina kwa kuandaa Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Intifada (mwamko) ya Palestina.
Mkutano wa kimataifa wa siku mbili kuhusu kuunga mkono mwamko wa Palestina unaanza leo hapa mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na washiriki kutoka nchi 80. Sayyed Nasrallah amesema mkutano huo unafanyika katika wakati muhimu wa mabadiliko ya sera za Marekani kuhusu kile kinachotajwa kuwa suluhisho la nchi mbili baina ya Palestina na Israel.