IQNA

Serikali ya Kenya yatakiwa kuzuia kusumbuliwa wasichana Waislamu wanaovaa Hijabu shuleni

11:39 - December 31, 2017
Habari ID: 3471334
TEHRAN (IQNA)-Baraza Kuu la Waislamu Kenya , Supkem, limetoa wito kwa serikali kuchukua hatua za kuzuia kusumbuliwa wasichana Waislamu wanaovaa Hijabu wakiwa shuleni.

Serikali ya Kenya yatakiwa kuzuia kusumbuliwa wasichana Waislamu wanaovaa Hijabu shuleni

Katika taarifa, katibu mwandalizi wa Supkem Abdullahi Salat ameitaka Wizara ya Elimu nchini Kenya kuchunguza suala la kusumbuliwa wanafunzi Waislamu wanaovaa Hijabu.

Kiongozi huyo wa Waislamu amelalamika kuwa, wanafunzi wa kike wanabughudhiwa na kudhalilishwa pamoja na kuwa mahakama imetoa hukumu ya kuruhusu wanafunzi kuvaa Hijabu wakiwa shuleni.

Salat amesema ni jambo lisilokubalika kwa shule kuwafukuza wanafunzi kwa sababu tu wameamua kuvaa Hijabu ambayo ni katika maamurisho ya dini ya Kiislamu.

Akizungumza huku shule zikitazamiwa kufunguliwa siku chache zijazo, afisa huyo wa Sukem ameitaka serikali kuzichunguza shule ambazo zinawabagua wanafunzi Waislamu wanaovaa Hijabu.

Katika hukumu iliyotoelwa Septemaba mwaka 2016 Mahakama ya Rufaa Kenya ilisema wanafunzi wa kike Waislamu wanaweza kuvaa Hijabu kama sehemu ya mavazi rasmi ya shule. Majaji waliotoa hukumu hiyo walitaka Wizara ya Elimu iweke kanuni mpya ambayo zitazishurutisha shule kuwaruhusu wanafunzi wasichana Waislamu kuvaa Hijabu pasina kubaguliwa.

Kesi ya kupinga uvaaji Hijabu shuleni ilikuwa imewasilishwa na shule inayofadhiliwa na Kanisa la Methodist katika eneo la Isiolo. Shule hiyo ilienda mahakamani baada ya Idara ya Elimu Kenya kusema wasichana Waislamu wanaweza kuvaa mitandio na suruali nyeupe kama sehemu ya mavazi rasmi ya shule.

/3677481

captcha