IQNA

Rais Hassan Rouhani
17:59 - November 24, 2018
News ID: 3471749
TEHRAN (IQNA)-Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyataka mataifa ya Waislamu kuungana na kusimama imara kukabiliana na siasa za chuki za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Akihutubia mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Kiislamu hapa Tehran, Rais Rouhani amesema, Waislamu hawana njia nyingine isipokuwa kuungana na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kupata ushindi dhidi ya Marekani na ubeberu wake.

Amesema, umoja na mshikamano baina ya nchi za Kiislamu unapaswa kuhesabiwa kuwa ni jukumu la kila mtu. Hata hivyo amekumbusha kuwa, umoja hauwezi kupatikana kwa maneno matupu na kusisitiza kwamba kuna wajibu wa kuchukuliwa hatua za pamoja za kivendo kufanikisha jukumu hilo.

Vile vile amesema katika hotuba yake hiyo kwamba, Iran inaiona Saudi Arabia kuwa ni ndugu yake na iko tayari kushirikiana na nchi hiyo kutatua matatizo yaliyopo.

Mkutano wa 32 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza hapa mjini Tehran ukiwa umewakusanya pamoja washiriki 350 kutoka nchi 100 tofauti duniani.

Mkutano huo wa siku tatu umefunguliwa leo Jumamosi chini ya kaulimbiu ya "Quds, mhimili wa umoja katika Ummah."

Mkutano huo hufanyika kila mwaka katika kipindi cha baina ya mwezi 12 na 17 Mfunguo Sita cha maadhimisho ya Maulidi na Siku ya Kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW na kinajulikana pia kwa jina la kipindi cha Wiki ya Umoja baina ya Waislamu.

3766535

Name:
Email:
* Comment: