IQNA

Kwa mnasaba wa Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW

Mkutano wa 34 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu kufanyika Tehran

14:53 - September 17, 2020
Habari ID: 3473178
TEHRAN (IQNA) – Mkutano wa 34 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu utafanyika Novemba 11-13 katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran.

Kwa mujibu wa taarifa mada ya mkutano huu itahusu ‘Ushirikiano wa Kiislamu Wakati wa Majanga na Maafa.”

Washiriki katika mkutano huo wametakiwa wawasilishe makala zao kabla ya Oktoba sita. Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu huandaliwa kila mwaka mjini Tehran na Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu.

Mkutano huo hufanyika kila mwaka kwa munasaba wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ni kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 za Mfunguo Sita Rabiu Awwal kipindi ambacho kinasadifiana na kuadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Bwana Mtume SAW. Kuhusiana na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia.

Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Shiia Ithanaashari linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo. Mitazamo hiyo miwili takribani pengo lake ni kipindi cha wiki moja. Kwa kuzingatia hali hiyo, Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (MA) Mwasisi na Mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akakitaja kipindi hiki cha wiki moja kuwa Wiki ya Umoja, ili Waislamu badala ya kuvutana na kuanza kukuza tofauti za tarehe za kuzaliwa Bwana Mtume SAW wakae pamoja na kujadili umuhimu wa umoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla.

3472579

captcha