IQNA

EU yatenga Euro Milioni 10 za utafiti kuhusu taathira ya Qur'ani Ulaya

20:50 - December 21, 2018
Habari ID: 3471780
TEHRAN (IQNA)-Umoja wa Ulaya (EU) umetangaza kutenga bajeti ya Euro Milioni 10 kwa ajili ya utafiti wa kina kuhusu namna Qur'ani Tukufu imeathiri utamaduni wa Ulaya.

Kwa mujibu wa taarifa, utafiti huo utasimamiwa na Bi. Mercedes García Arenal mtaalamu wa Uislamu na ambaye ni mtafiti katika Taasisi ya Lugha na Tamaduni za Mediterranean na Mashariki ya Karibu katika Baraza Kuu la Utafiti wa Kisayansi (CSIC) la Uhispania. García Arenal amesema msingi wa nadharia ya utafiti huo ni kuwa Qur'ani Tukufu imekuwa na nafasi muhimu katika ustawi wa kifikra na kidini barani Ulaya. Amesema utafiti huo utaangazia namna Qur'ani ilivyotarjumiwa, kuhaririwa, kuchapishwa, kusambazwa na hatimaye taathira na matumizi yake ya kidini na kiutamaduni barani Ulaya kuanzia Zama za Kati (Middle Ages) hadi Zama za Mwamko (Enlightenment Era).

Halikdhalika utafiti huo utalenga kuangazia ni kiasi gani Qur'ani Tukufu imeweza kuathiri fikra za Waislamu na Wakristo wa zama hizo mbili na zama za sasa barani Ulaya. Mradi huo pia utachunguza ni vipi Qur'ani imeathiri mitazamo ya Mayahudi na wasiomuamini Mungu barani Ulaya.

Hayo yanajiri wakati ambao  uchunguzi wa Shirika la Pew uliotangazwa Novemba mwaka 2017 umebaini kuwa idadi ya Waislamu barani Ulaya imekadiriwa kuongezeka kutoka milioni 25 hivi sasa hadi kufikika milioni 76 ifikapo mwaka 2050.

3774176/

captcha