IQNA

Idadi ya Waislamu Marekani Kuongezeka Maradufu Ifikapo Mwaka 2050

10:43 - January 04, 2018
Habari ID: 3471342
TEHRAN (IQNA)-Idadi ya Waislamu wanaoishi nchini Marekani inatazamiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050 na hivyo kuufanya Uislamu kuwa dini ya pili kwa ukubwa nchini humo.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew na kutangawa Jumatano, katika kipindi cha muongo moja uliopita, idadi ya Waislamu Marekani imeongezeka kwa karibu watu milioni moja na iwapo mkondo huo utaendelea,  basi Uislamu utachukua nafasi ya sasa ya Uyahudi kama dini ya pili kwa ukubwa nchini humo ifikapo mwaka 2040.

Kituo cha Utafiti cha Pew kinasema ni vigumu kubaini kikamilifu idadi ya Waislamu wanaoishi Marekani kwa sababu Idara ya Sensa nchini humo haiulizi kuhusu dini wakati wa sensa. Uchunguzi wa Pew uliochapishwa mwaka jana ulibaini idadi ya Waislamu Marekani mwaka 2015 ilikuwa  ni milioni 3.3 au takribani asilimia moja ya watu wote milioni 322 nchini humo.

Kwa mujibu wa Pew, mwaka 2007 kulikuwa na Waislamu takribani milioni 2.3 waliokuwa wakiishi Marekani na idadi hiyo inaongezeka kwa kasi ikilinganishwa na jamii ya Mayahudi.

Makadirio yanaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2050, idadi ya Waislamu itaongezeka na kufika milioni 8.1 au asilimia 2.1 ya idadi yote ya Wamarekani-na hiyo ni mara mbili ya idadi yao hivi sasa. Uchunguzi umebaini kuwa idadi ya Waislamu Marekani huongezeka kwa takribani laki moja kwa mwaka.

Pamoja na kuwepo ongezeko la chuki dhidi yao, Waislamu wanazidi kuongezeka na hilo linaashiria kuwa kuna watu wengi ambao wanafanya utafiti na kuikumbatia dini tukufu ya Kiislamu maishani huku wakipuuza kauli za kichochezi.

Hivi karibuni pia, Kituo cha Pew kilitangaza kuwa, idadi ya Waislamu barani Ulaya inakadiriwa kuongezeka kutoka milioni 25 hivi sasa hadi kufikika milioni 76 ifikapo mwaka 2050.

3679087

captcha