IQNA

22:25 - June 24, 2019
News ID: 3472016
TEHRAN (IQNA) – ‘Muamala wa Karne’ ambao umependekezwa na Marekani kwa lengo la kuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel na kukandamiza ukombozi wa Palestina unaendelea kupingwa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa hila ya serikali ya Marekani ya kutaka kutekeleza mpango kwa jina la Muamala wa Karne haitafanikiwa.

Hazem Qassim amesema kuwa mapambano dhidi ya maghasibu wanaoikalia kwa mabavu Palestina yataendelea hadi nchi huru ya Palestina itakapoundwa huku mji mkuu wake ukiwa Baitul Muqaddas. Msemaji wa Hamas ameyasema hayo katika radiamali yake kwa hatua ya kuwekwa wazi mikakati mipya kuhusu mpango huo wa Marekani na Wazayuni wa Muamala wa Karne. Wakati huo huo Yuval Steinitz Waziri wa Nishati wa utawala wa Kizayuni amekaribisha maelezo mapya yaliyowekwa wazi katika mpango huo wa Muamala wa Karne.

Udhalilishaji

Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Muqawama Hizbullah nchini Lebanon amesema kuwa, mtazamo wa Marekani kwa wananchi wa Palestina kuwa ni watu masikini ambao matatizo yao yanatatuliwa tu kwa fedha, ni udhalilishaji mkubwa kwa watu wa taifa hilo.

Ibrahim Amin al-Sayyed amesema kuwa kadhia ya Palestina ni kadhia kubwa katika ulimwengu wa leo, lakini kitendo cha Marekani kuwapuuza Wapalestina, haki ya uepo wao na haki yao ya kisiasa, kimeifanya iwatazame Wapalestina kama ni kundi la watu masikini ambao matatizo yao yanaweza kutatuliwa kupitia kikao cha mjini Manama, Bahrain. Kwa upande wake 'Kundi la Utendaji la Lebanon na Palestina' inalofuatilia kadhia ya wakimbizi wa Kipalestina, limefanya kongamano nchini Lebanon kwa lengo la kutangaza msimamo wake kuhusiana na kadhia ya Muamala wa Karne. Kikao cha mjini Manama chenye lengo la kuchunguza njia za utekelezaji wa hatua ya kwanza ya mpango wa Kimarekani na utawala wa Kizayuni wa Muamala wa Karne, kuhusiana na kadhia ya Palestina kitaanza Jumanne ya kesho na kumalizika silu ya Jumatano.

Wanazuoni walaani njama

Wakati huo huo, Wanazuoni na wasomi wa Kiislamu wa Lebanon na Palestina wamelaani njama ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina iliyopewa jina la 'Muamala wa Karne'.

Wanazuoni hao chini ya Bodi ya Maulamaa wa Kiislamu ya Palestina na Jumuiya ya Wanazuoni wa Lebanon wamekutana katika mji wa Saida nchini Lebanon, ambapo sambamba na kusisitizia udharura wa umoja wa umma wa Kiislamu, wameutaka ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu kutounga mkono mpango huo wa Washington na Tel Aviv wa kuitokomeza kadhia ya Palestina unaotazamiwa kuzinduliwa 25 Juni.

Kadhalika wasomi hao wa Kiislamu wa Lebanon na Palestina wametangaza kuwa suluhu ya mgogoro wa Wapalestina na Israel ni kuruhusiwa wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao za jadi zilizoghusubiwa na Wazayuni.

Haya yanajiri huku maelfu ya wananchi wa Morocco wakifanya maandamano makubwa ya kupinga mkutano huo wa kufungua mpango wa Marekani wa Muamala wa Karne wa kuangamiza kadhia ya Palestina.

Dola bilioni 50

Inafaa kuashiria kuwa katika miezi ya hivi karibuni, viongozi wa serikali ya Trump wamethibitisha kwamba, katika mkutano wao wa fursa za kiuchumi mjini Manama, mji mkuu wa Bahrain, kutazinduliwa pia hatua ya kwanza ya kiuchumi ya Muamala wa Karne. Kongamano la Manama limepangwa kufanyika kati ya tarehe 25 na 26 za mwezi huu katika mji mkuu wa Bahrain, Manama. Katika miaka ya hivi karibuni utawala wa Aal-Khalifa, umejiunga na Saudi Arabia katika kuimarisha sana uhusiano wake na utawala haramu wa Kizayuni.

Jared Kushner mkwe na mshauri wa Rais Donald Trump wa Marekani juzi alieleza kuwa marhala ya kwanza ya mpango wa Muamala wa Karne inalenga kuwekeza dola bilioni 50 huko katika ardhi za Palestina, Misri, Jordan na Lebanon.

Mpango huo uliopendekezwa na Marekani kwa jina la "Muamala wa Karne" unajumuisha kuiunganisha kikamilifu Quds Tukufu na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, kuviunganisha vitongoji vilivyopo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na utawala huo, kufuta kikamilifu haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi za mababu zao na kuainisha eneo la Abu Dis kama mji mkuu wa nchi ya Palestina.

Mpango huo umepingwa vikali na Waislamu kote duniani na wananchi wa Palestina; huku ukizidisha ghasia na mapigano kati ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni na Wapalestina khususan katika Ukanda wa Ghaza.

3821919

Name:
Email:
* Comment: