IQNA

Sheikh Issa Qassim
11:50 - June 25, 2019
News ID: 3472017
TEHRAN (IQNA) - Mwanazuoni maarufu wa Kiislamu nchini Bahrain, Ayatullah Sheikh Isa Qassim amelaani vikali hatua ya utawala wa Manama kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kibiashara linalotazamiwa kuanza leo nchini humo kwa shabaha ya kuzindua mpango wa 'Muamala wa Karne'.

Ameongeza kuwa mpango huo wa Rais Donald Trump wa Marekani unakusudia kuwapokonya Wapalestina haki zao zote na kuuza kila kitu kinachomilikiwa nao yakiwemo maeneo matakatifu.

Sheikh Isa Qassim ameyasema hayo katika Mkutano wa Muqawama (Mapambano ya Kiislamu) wa Vijana katika mji mtakatifu wa Qum, kusini mwa Tehran hapa nchini Iran Jumatatu usiku.

Akizingumza katika hafla hiyo Sheikh Qassim ambapo amebainisha kuwa, ulimwengu wa Kiislamu hauna changuo jingine ghairi ya kuukataa katakata mpango huo wa 'Muamala wa Karne'.

Mwanachuoni huyo wa Bahrain amesisitiza kuwa, kuukataa mpango huo wa Marekani na Wazayuni dhidi ya Wapalestina ni kukataa utumwa na kukukumbatia uhuru.

Ayatullah Sheikh Issa Qassim amesema kitendo cha kuwakaribisha nchini Bahrain Wazayuni ni hatua moja kuelekea katika njia ya kujidhalilisha kwa adui mkubwa zaidi kwa ulimwengu wa Kiislamu.

Mwanachuoni huyo maarufu wa Kiislamu nchini Bahrain amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndiye adui nambari moja wa ulmwengu wa Kiislamu ambaye hapaswi kukaribishwa, kupokewa wala kupewa mkono.

Sheikh Isa Qassim amehudhuria Mkutano wa Pili wa Muqawama wa Vijana mjini Qum, ambao umewaleta pamoja vijana kutoka nchi 60 duniani ambao wamekumbuka na kuwaenzi vijana waliouawa shahidi wakipambana na udikteta wa utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain.

Jared Kushner mkwe na mshauri wa Rais Donald Trump wa Marekani juzi alieleza kuwa marhala ya kwanza ya mpango wa Muamala wa Karne inalenga kuwekeza dola bilioni 50 huko katika ardhi za Palestina, Misri, Jordan na Lebanon.

Mpango huo uliopendekezwa na Marekani kwa jina la "Muamala wa Karne" unajumuisha kuiunganisha kikamilifu Quds Tukufu na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, kuviunganisha vitongoji vilivyopo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na utawala huo, kufuta kikamilifu haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi za mababu zao na kuainisha eneo la Abu Dis kama mji mkuu wa nchi ya Palestina.

Mpango huo umepingwa vikali na Waislamu kote duniani na wananchi wa Palestina; huku ukizidisha ghasia na mapigano kati ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni na Wapalestina khususan katika Ukanda wa Ghaza.

3822117

Name:
Email:
* Comment: