IQNA

12:24 - July 16, 2019
News ID: 3472046
TEHRAN (IQNA) - Wabunge katika Kongresi ya Marekani ambayo walidhalilishwa na Rais Donald Trump wa nchi hiyo wamesema hawatatishika.

Wabunge wanawake waliolengwa na Trump kwa matamshi hayo ya chuki za kibaguzi ambao ni Ilhan Omar aliyezaliwa Somalia, Rashida Tlaib mwenye asili ya Palestina, Alexandria Ocasio-Cortez ambaye asili yake ni Puerto Rico na Ayanna Pressley, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika wamejibu matamshi hayo ya kibaguzi ya Trump na kusema katika taarifa kuwa, "Matamshi ya Trump ni mbinu ya upotoshaji, ili tusiendelee kukosoa utawala wake wa kifisadi, wa kibaguzi na uliofeli."
Wawakilishi hao wa Kongresi ya Marekani wamesema silaha aliyobakia nayo Trump ni ubaguzi tu.
Hivi karibuni, Trump aliwatukana matusi ya kibaguzi wabunge wanawake wa chama wa Democrat katika Kongresi ya Marekani kwa kuwaambia, wao si Wamarekani na kuwataka warudi nchi walizotoka.
Trump ametoa matusi hayo ya kibaguzi kupitia ukurasa wake wa Twitter kwa kuandika ujumbe usemao: "Ni jambo la kuvutia mno kuona wabunge wanawake 'wapenda maendeleo' wa Democrat katika Kongresi, ambao kimsingi wamekuja kutoka nchi ambazo serikali zao ni majanga matupu, zikiwa ni miongoni mwa serikali mbaya zaidi, fisadi zaidi na mbovu zaidi duniani (kwa sharti kama hizo serikali zenyewe zitakuwepo katika nchi hizo), sasa wanawapazia sauti na kwa ukali wananchi wa Marekani, ambayo ni nchi kubwa zaidi na yenye nguvu zaidi duniani, kuwaambia ni vipi serikali yetu inapasa iendeshwe."
Katika ujumbe wake huo, Trump ameongezea kwa kusema: "Kwa nini hawarudi na kwenda kusaidia kurekebisha maeneo walikotoka yenye uhalifu? Kisha rudini muje kutuonyesha vipi mumeifanya kazi hiyo. Sehemu hizo zinahitaji sana msaada wenu. Inapasa muondoke haraka iwezekanavyo."
Japokuwa hakuwataja kwa majina, wabunge wanawake aliowalenga Trump kwa matamshi hayo ya chuki za kibaguzi ni Ilhan Omar , RashidaTlaib , Alexandria Ocasio-Cortez ambaye na Ayanna Pressley.
Wakati huo huo, Viongozi na wanasiasa kote duniani wameendelea kumlaani Rais Donald Trump wa Marekani kwa kuwadhalilisha na kuwatukana matusi ya kibaguzi wabunge wanawake wa chama cha Democrat katika Kongresi ya Marekani.
Waziri Mkuu anayeondoka wa Uingereza, Theresa May amesema, "Matamshi ya Trump ya kuwadhalilisha wabunge wanawake wa Kongresi ya nchi hiyo hayakubaliki. Lugha iliyotumika katika ujumbe huo wa Trump haikubaliki."
Naye Jacinda Ardern, Waziri Mkuu wa New Zealand ambaye anasifika kote duniani kwa sera zake za kuwaunga mkono wahajiri na kuwatetea watu wa jamii za walio wachache nchini humo amesema, "Kwa kawaida huwa siingilii siasa za watu wengine, lakini ni wazi kuwa kama walivyofanya watu wengine, na mimi siiungi mkono kauli hiyo ya kibaguzi ya Trump."
Wakati huohuo, Ibrahim Milhim, msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kauli ya Trump ni tusi kwa ofisi ya rais na mfumo wa sheria za Marekani.

3468974

Name:
Email:
* Comment: