IQNA

12:29 - August 23, 2019
News ID: 3472096
TEHRAN (IQNA) – Mcheza soka mstaafu wa kulipwa barani Ulaya, Frederic Oumar Kanoute, mwenye asili ya Afrika anaongoza mkakati wa kujenga msikiti huko Sevilla nchini Uhispania.

Kanoute ana asili ya Mali na uraia wa Ufaransa na aliwahi kuchezea vilabu mashuhuri vya Ulaya kama vile Lyon ya Ufaransa, Tottenham Hotspur na West Ham za Uingereza na Sevilla katika ligi kuu ya Uhispania maarufu kama La Liga.

Mwanasoka huyo aliyestaafu, ambaye aliwahi kuifungia Klabu ya Sevilla mabao 89 katika mechi 209, sasa anaongoza kampeni ya kujenga msikiti katika mji huo, ambao kwa miaka 700 umekuwa bila msikiti.

Uhusiano wa Kanoute na Msikiti wa Seville ulianza mwaka 2007. Wakati huo Waislamu katika mji huo walitakiwa waondoke katika jengo ambalo walikuwa wamelikodi na kulitumia kama msikiti kutokana na kuwa, walikuwa wameshindwa kulipa kodi.

Baada ya habari hizo kumfikia Kanoute alitoa mchango binafsi wa dola laki saba na kulinunua jengo hilo ili Waislamu wa Seville wawe na eneo la daima la kutekeleza ibada zao pasina kufadhaishwa.

Kanoute, ambaye pia aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Mali, anasema hakutaka amali yake hiyo njema itangazwe hadharani lakini baada ya siku kadhaa habari hizo zilisambaa katika vyombo vya habari.

Waislamu mjini Saville walimpongeza sana Kanoute kwa ukarimu wake kwani kama hangetoa mchango wake hawangekuwa na eneo la kutekeleza ibada na kujumuika.

Kutokana na ongezeko kubwa la Waislamu mjini Seville, hivi sasa jengo hilo linahitaji ukarabati mkubwa ili liwe msikiti kamili. Kutokana na hali hiyo, Kanoute ameanzisha kampeni mpya ya kukusanya michango ili kuwezesha jingo hilo kuhudumia idadi kubwa ya Waislamu sevile.

Mwezi Machi mwaka huu, Kanoute alizindua kampeni katika mitandao ya kijamii kwa anuani ya #Kanoute4SevilleMosque kwa lengo la kuchangisha dola $ 350,000 ili kujenga jingo la ghorofa tatu lenye msikiti na sehemu ya kuegeshea magari.

Akiwa anashirikiana na Ibrahim Hernandez na Luqman Nieto, rais na makamu wa Rais wa Taasisi ya Msikiti wa Sevilla, wanataraji kuwaleta Waislamu pamoja ili kuujenga msikiti huo.

Mwezi wa Ramadhani mwaka huu walifanikiwa kukusanya nusu ya fedha wanazohitaji na wangali wanaendeleza kampeni hiyo.

Frederic Oumar Kanoute alizaliwa mjini Lyon Ufaransa Desemba 2 mwaka 1977 ambapo mama yake ni Mfaransa na baba yake ni Mmali.

Baada ya kufanya uchunguzi na utafiti wa kina, mwaka 1997 alitambua Uislamu kama njia ya haki na hivyo akawa Mwislamu. Katika kipindi chote chake kama mcheza soka wa kulipwa, Kanoute alifungamana kikamilifu na itikadi ya Kiislamu na alikuwa mfano wa kuigwa na vijana wengi.

Inafaa kuashiria hapa kuwa Uhispania na Ureno ni nchi zilizokuwa zinatawaliwa na Waislamu kati ya miaka 711 and 1492 Miladia wakati huo eneo hilo likijulikana kama Al-Andalus na mji wa Seville uko katika eneo hilo. Katika karne ya 8 na 9 polepole sehemu kubwa ya Wakristo walipokea Uislamu uliokuwa dini tawala. Mnamo mwaka 1100 takriban 80% za wakazi walikuwa Waislamu kabla ya hali kubadilika katika karne zilizofuata.

3836573

Name:
Email:
* Comment: