IQNA

Al Azhar yakosoa marufuku ya Hijabu katika shule Uhispania

21:23 - November 06, 2021
Habari ID: 3474523
TEHRAN (IQNA)- Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri kimekosoa uamuzi wa shule moja Uhispania kupiga marufuku vazi la Hijabu na kutaja kitendo hicho kuwa ni ubaguzi.

Ofisi ya Al Azhar ya Kufuatilia Vitendo vya Chuki Dhidi ya Uislamu (Islamophibia) imetoa taarifa na kulaani kitendo cha shule kumfukuza mwanafunzi msichana Muislamu kwa sababu tu kuwa anavaa Hijabu.

Taarifa hiyo imesema kitendo kama hicho cha kibaguzi ni tishio kwa maisha ya pamoja kwa amani katika jamii.

Gazeti la Uhispania la Periodico CLM limeandika kuwa kumefanyika maandamano ya kumuunga mkono mwanafunzi huyo aliyetimuliwa shuleni.

Waandamanaji walibeba mabanga na kutoa nara za kupinga vitendo vya ubaguzi dhidi ya Waislamu.

Haya yanajiri katika hali ambayo Uislamu una historia ndefu nchini Uhispania ambapo nchi hiyo iliwahi kutawaliwa kwa karne kadhaa na Waislamu.

Al-Andalus ilikuwa jina la Kiarabu la sehemu za Rasi ya Iberia (Uhispania na Ureno za leo) zilizotawaliwa kwa karne kadhaa na Waislamu kati ya miaka 711 and 1492 Miladia.

Eneo hilo ilikuwa chini ya falme na watawala mbalimbali kwanza chini ya Banu Umayya, halafu Ukhalifa wa Cordoba (929-1031) na baadaye chini ya milki mbalimbali hasa Wamurabitun (Almoravi) (1073-1147) na Wamuwahidun (Almohad) (1125-1269) kutoka Morocco.

/4011024

captcha