IQNA

Rais Rouhani katika Umoja wa Mataifa
7:55 - September 26, 2019
News ID: 3472147
TEHRAN (IQNA) -Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ni jambo lisiloyumkinika kwa taifa hili kufanya mazungumzo na adui likiwa chini ya mashinikizo na vikwazo vya kidhalimu na vilivyo kinyume cha sheria.

Rais Rouhani amesema hayo Jumatano katika hotuba yake mbele ya mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kusisitiza kuwa, licha ya mashinikizo na vikwazo vya maadui, lakini uchumi wa Iran unazidi kustawi na kuimarika.

Amesema licha ya uchumi wa kigaidi wa kiwango cha juu wa Marekani dhidi ya Iran, lakini Wairani wamesimama ngangari mkabala ya ukatili huo. Amesema, "Wenye ndoto ya kupata jibu la NDIO kutoka kwa Iran kwa ajili ya kuitikia mwito wao wa mazungumzo, wanapaswa kufahamu kuwa, njia pekee ya kupata jibu hilo ni kufuata muongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei wa kurejea na kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA."

Kuhusu hali ya eneo la Mashariki ya Kati, Dakta Rouhani amebainisha kuwa, moto wa ugaidi, vita, uvamizi, uporaji wa ardhi na uchupaji mipaka unaliteketeza eneo hili. Amesisitiza kuwa Marekani ni muungaji mkono wa ugaidi na misimamo ya kufurutu ada katika eneo, na kwa msingi huo haina uwezo wala wajibu wa kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazolikabili eneo.

Rais Rouhani amesema Marekani sio mlinzi wala mtetezi wa taifa lolote katika Mashariki ya Kati. Amebainisha kuwa, "Marekani imeshindwa kupatia ufumbuzi migogoro katika nchi za Afghanistan, Iraq na Syria na hivyo haipaswi kuwa na nafasi yoyote katika kupunguza taharuki na kuleta amani katika eneo." Kadhalika Dakta Rouhani amelaani vikali mashambulizi ya kikatili ya muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen, sambamba na kubainisha uungaji mkono wa Iran kwa kadhia ya Palestina.

Amesisitiza kuwa, "Kuimarisha usalama, amani, uthabiti, na maendeleo katika Ghuba ya Uajemi na Lango la Bahari la Hormuz ni katika majukumu ya kihistoria ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Huku akizikaribisha nchi za eneo kuunga mkono Mpango wa Amani wa Hormuz, Rais Rouhani ameongeza kuwa, "natoa wito kwa nchi zote ambazo zinahusika kwa njia moja au nyingine na hali ya amani na usalama na amani katika Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormoz kujiunga na muungano wa Jitihada za Amani katika Hormoz."

3845023

Name:
Email:
* Comment: