IQNA

18:53 - October 26, 2019
News ID: 3472187
TEHRAN (IQNA) – Msikiti wa Jamia katika mji wa Nairobi, Kenya umefungua milango yake kwa wasiokuwa Waislamu kuutembelea ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwaka wa 94 wa ujenzi wake.

Kwa mujibu wa taarifa, siku ya Jumamosi 26 Oktoba, Msikiti wa Jamia ambao ni msikiti mkubwa zaidi nchini Kenya, ulifungua milango yake kwa umma pasina kujali dini au itikadi.

Wageni waliofika katika msikiti huo walitembezwa katika maeneo yote huku wakipewa maelezo kuhusu yanayojiri ndani ya msikiti kila siku. Aidha walipata fursa ya kuuliza maswali sambamba na kushiriki katika mijadala mbali mbali. Halikadhalika waliotembelea msikiti walipata fursa ya kuona namna Waislamu wanavyoswali na kisha walipewa vitabu vilivyo na maelezo kuhusu Uislamu na Waislamu.

Septemba  mwaka jana pia, Msikiti wa Jamia ulikuwa mwenyeji wa wahubiri wa Kikristo wakati wa Sala ya Ijumaa ili kuimarisha maelewano baina ya Wakristo na Waislamu nchini humo.

Aidha mwezi Mei mwaka huu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Rais Uhuru Kenyatta alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo kutembelea msikiti na kujumuika na Waislamu wakati wa Sala na Futari.

Hatua ya Msikiti wa Jamia kufungua milango yake kwa watu wote ni kujaribu kuwasilisha taswira sahihi kuhusu Uislamu katika nchi hiyo na kuondoa dhana potovu zilizokoko kuhusu Uislamu na Waislamu.

3469743

Name:
Email:
* Comment: