IQNA

Chuo Kikuu cha Al Mustafa (SAW) chalaani kimya cha kimataifa kuhusu masaibu ya Sheikh Zazaky

22:23 - December 17, 2019
Habari ID: 3472285
TEHRAN (IQNA) – Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al Mustafa SAW kimetoa taarifa na kulaani kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu kuendelea kushikiliwa kinyume cha sheria kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) Sheikh Ibrahim al-Zakzaky na mke wake, pamoja na kuwa hali yao ya kiafya imezorota.

Katika taarifa, chuo hicho kimesema Sheikh Zakzaky na mke wake wana hali mbaya ya kiafya huku watoto wao kadhaa pamoja na wanachama wa IMN wakiwa wameuawa shahidi katika oparesheni za jeshi la Nigeria. Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al Mustafa SAW kimesema hayo yanajiri katika hali ambayo mashirika ya kimatiafa na yale yanayojinadi kutetea haki za binadamu yakiwa kimya.

Chuo hicho kimetoa wito kwa wapenda haki na uhuru kote duniani kusimma na kupinga dhulma inayotendwa dhidi ya Sheikh Zakzaki na mke wake.  Aidha Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Al Mustafa SAW kimetoa wito kwa wakuu wa Nigeria kuwaachilia huru wawili hao ili wapate matibabu.

Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky, 66, na mkewe walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kushambulia Hussainiyah iliyoko katika mji wa Zaria. Katika shambulio hilo, Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria wasiopungua 1,000, wakiwemo wana watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi.

Baada ya jitihada kubwa, maandamano ya kila pembe na mashinikizo mengi ya ndani na kimataifa, mnamo mwezi Agosti, mahakama ya Nigeria iliruhusu Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wapelekwe India kutibiwa, lakini kutokana na matatizo na vizuizi vilivyowekwa na maafisa wa usalama walioandamana naye, kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe waliamua kurudi Nigeria baada ya kukaa India kwa muda wa siku mbili tu pasi na kupatiwa matibabu.

Kabla ya hapo, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilikuwa imefichua kwamba, serikali ya nchi hiyo imekula njama ya kumuua Sheikh Zakzaky kwa kutumia mbinu tofauti ikiwemo ya kumpa sumu.

3864674

captcha