IQNA

Kwa mnasaba wa Krismasi

Kiongozi Muadhamu awataka Wakristo washikamane na mafundisho ya Nabii Isa Masih AS

15:22 - December 25, 2019
Habari ID: 3472302
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewanasihi wafuasi wa dini ya Kikristo wafungamane na vitendo vyema kama walivyoelekezwa na Nabii Issa Masih (Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-AS-).

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika ujumbe wake aliotuma kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mazazi ya Nabii Issa (AS), yanayoadhimishwa hii leo na Wakristo kote duniani.

Katika ujumbe huo aliotuma kwenye ukurasa wake wa Twitter, Kiongozi Muadhamu ameandika: Miongozo ya Nabii Issa Bin Maryam (AS), ni miongozo ya kuabudiwa Mungu mmoja, na kupambana na Mafarao na madhalimu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa, "Kumfuata #YesuKristo kuna maana ya kufungamana na vitendo vyema na kujiweka mbali na nguvu za upotofu, na inatarajiwa kuwa, Waislamu na Wakristo katika kona zote za dunia watashikamana na mafunzo hayo makubwa ya Nabii Issa (AS) katika maisha na matendo yao."

Inafaa kuashiria hapa kuwa, siku kama ya leo miaka 2020 iliyopita, Nabii Issa Masih (AS) alizaliwa katika mji wa Bait Laham (Bethlehem) huko Palestina. Nabii Issa Masih alipewa uwezo na Mwenyezi Mungu wa kufanya miujiza mingi. Issa Masih AS alianza kuzungumza akiwa mdogo na kujibashiria unabii. Mwenyezi Mungu anaashiria tukio la kuzaliwa kwa Nabii Issa katika Qur'ani Tukufu katika Suratu Aal Imran aya ya 45 kwa kusema: Kumbukeni waliposema Malaika: "Ewe Mariam! Mwenyezi Mungu anakubashiria mwana kwa neno litokalo kwake; jina lake ni Masih, Issa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera na miongoni mwa waliokurubishwa." Inafaa kuashiria hapa kwamba, tarehe 25 Disemba kila mwaka inajulikana kote duniani hasa kwa Wakristo kuwa ni Sikukuu ya Krismasi. IQNA inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa wafuasi wa kweli wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu.

3866515

captcha