IQNA

17:23 - December 25, 2019
News ID: 3472303
TEHRAN (IQNA) -Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa kheri na pongezi kwa Wakristo kwa mnasaba wa kukumbuka kuzaliwa Nabii Isa Masih (Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-AS-) inayoadhimishwa leo na ambayo ni maarufu kama Krismasi.

Akizungumza katika kikao cha baraza la mawaziri hapa mjini Tehran leo Jumatano, Rais Rouhani amebaini kuwa: "Katika siku yenye baraka ya kukumbuka kuzaliwa Nabii Isa Masih, Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, natoa salamu za pongezi kwa Wakristo wote duniani na pia kwa Wakristo hapa kwetu Iran. Pia kwa mnasaba wa siku hii natoa salamu kwa Waislamu wote kwani siku ya kukumbuka kuzaliwa Nabii Isa Masih ni siku kuu ya Idi kwa Waislamu na Wakristo kwa sababu alikuwa miongoni mwa Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu."

Rais Rouhani amesema Nabii Isa Masih (AS) alikuwa Mtume wa nuru, Mtume wa rahma, Mtume wa urafiki na mawada na mapenzi miongoni mwa watu. Rais wa Iran ameongeza kuwa, Qurani Tukufu imetukumbusha sisi Waislamu kuwa tuna nukta muhimu za pamoja na Ahlul Kitab au Watu wa Kitabu (Wakristo na Mayahudi) na tunapaswa kuzingatia nukta hizo na kuhusiana na hilo ameashiria aya ya 64 ya Suurat Al 'Imran katika Qur'ani Tukufu inayosema: "Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi."

Rais wa Iran amesema katika aya hii Allah SWT anamtaka Mtume Muhammad SAW awaite Ahlul Kitab kwa msingi wa nukta za pamoja baina ya Ahlul Kitab na Waislamu. Rais Rouhani amesema kunapaswa kuwa na umoja na mshikamano baina ya Waislamu na pia baina ya Waislamu na Wakristo kwa msingi wa mafundisho ya Uislamu.

Kuhusu kuishi kwa maelewano na Wakristo, Rais Rouhani ameashiria aya ya 46 ya Suurat Al A'nkabut inayosema:  " Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao."

Rais wa Iran ametoa wito wa kuzingatiwa mafundisho ya Qur'ani katika kuamiliana na Ahul Kitab na kuishi nao kwa amani na maelewano.

3866589/

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: