IQNA

Msomi wa Al Azhar awakosoa wanaoharamisha salamu za Krismasi

18:54 - January 05, 2022
Habari ID: 3474771
TEHRAN (IQNA)- Msomi mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Al Azhar amezitaja kuwa zisizo na msingi Fatwa za kupiga marufuku Waislamu kuwatumia Wakristo salamu za Krismasi.

Akizungumza na Televisheni ya Misri ya el Balad Sheikh Ahmed Omar Hashim, mwanachama wa Baraza la Fatwa la Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar amesema kubadilishana salamu na hisia nzuri baina ya Waislamu na wasio kuwa Waislamu ni jambo linalotakiwa.

Amesema Allah SWT hajawaharamisha Waislamu kuwatendea mema wasiokuwa Waislamu. Mwanazuoni huyo amesema Sirah ya Mtume Muhammad SAW inaoneysha haja ya  kuwepo maelewano baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu.

Halikadhalika amesema Mtume Muhammad SAW hakufunga mlango wa kuwatendea mema na kuwasaidia wasiokuwa Waislamu.

Sheikh Omar Hashim amesisitiza kuwa, yeyote atakayetoa Fatwa au amri ya kuwakataza Waislamu kuwapongeza wasiokuwa Waislamu katika siku kuu kama vile Krismasi na mwaka mpya basi si msomi wa Kiislamu.

Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya wahubiri Misri kutoa Fatwa kuwa ni haramu kwa Waislamu kuwatakia Wakristo Krismasi njema.

4026199

captcha