IQNA

Wananchi wa Yemen waandamana kuulaani "Muamala wa Karne"

22:28 - January 31, 2020
Habari ID: 3472424
Wananchi wa Yemen wamefanya maandamano makubwa ya kulaani njama mpya za Marekani dhidi ya taifa madhlumu la Palestina na wamelaani vikali mpango wa Donald Trump wa "Muamala wa Karne."

Televisheni ya Almasirah ya Yemen imetangaza habari hiyo leo Ijumaa na kuripoti kuwa, maandamano makubwa yamefanyika katika miji  Sanaa, Sa'ada na Al Hudaidya ambapo waandamanaji wamepiga nara za "Palestina ndiyo kadhia yetu kuu" na "hatuukubali muamala wa karne."

Kama ilivyo maarufu kwao, leo pia wananchi wa Yemen wamewatangazia walimwengu jinsi wanavyoguswa na kadhia ya Palestina na namna mazingira yoyote yale yasivyoweza kuteteresha msimamo wao thabiti wa kuihami Palestina.

Mpango wa Muamala wa Karne uliopendekezwa na Marekani unajumuisha kukabidhiwa kikamilifu Israel mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, vitongoji vilivyoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan vyote ipewe Israel, Wapalestina wasiwe na haki ya kurejea kwenye ardhi za mababu zao na makundi ya muqawama wa Palestina yapokonywe silaha ili kusiwe na jambo lolote linalohatarisha usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Siku ya Jumanne, rais wa Marekani, Donald Trump alizindua mpango huo akiwa pamoja na waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu. Trump alizindua mpango huo wa kidhulma baada ya kufanya mazungumzo pia na Benny Gantz, mkuu wa Muungano wa Blu na Nyeupe wa utawala pandikizi ambaye ni mpinzani mkuu wa Benjamin Netanyahu katika siasa za hivi sasa za Israel.

3875374

captcha