IQNA

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yapinga 'muamala wa karne' yaunga mkono Wapalestina

17:31 - February 01, 2020
Habari ID: 3472429
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amekosoa tangazo la mpango wa Marekani na Israel unaojulikana kama 'muamala wa karne' kwa ajili ya kutatua kadhia ya Palestina na kusema nchi za Kiarabu katu hazitaliacha taifa la Palestina peke yake.

Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema mpango huo uliotangazwa na rais wa Marekani unapaswa kupingwa vikali na nchi za Kiarabu. Katika taarifa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema: "Utawala wa Kizayuni umebuni mpango wa 'muamala wa karne' ili kutekeleza njama zake yaani kuunganisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) sambamba na kuangamiza malengo ya taifa la Palestina."

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas akiwa safarini mjini Cairo, amezungumza katika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ametoa wito kwa nchi za Kiarabu kuchukua msimamo wa pamoja kupinga 'muamala wa karne'.

Siku ya Jumanne iliyopita, Rais Donald Trump wa Marekani akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu aliamua kuchukua hatua ya upande mmoja, bila kujali kugonga mwamba juhudi zake za miezi kadhaa za kutafuta uungaji mkono wa kieneo na kimataifa pamoja na ridhaa ya mirengo ya Palestina, ya kuzindua mpango wa Kizayuni alioupa jina la "Muamala wa Karne".

Mpango huo wa kihaini unaokidhi matakwa ya utawala haramu wa Israel na kufuta haki za wananchi madhulumu wa Palestina umeandaliwa na serikali ya Marekani kwa ushirikiano na maafikiano na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu na Oman.

Kikao cha dharura cha waziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kimefanyika leo kufuatia ombi la Palestina.

3875655

captcha