IQNA

Zarif: Kusiwe na ubaguzi katika wanaadamu kusaidiana

7:59 - March 13, 2020
Habari ID: 3472560
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewasilisha orodha ya vifaa vya kitiba ambavyo Iran inahitajia kwa dharura ili kukabiliana na janga la ugonjwa wa COVID-19 au Corona.

Katika ujumbe aliondika katika ukurasa wake wa Twitter Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameandika: "Wanaadamu hawapasi kubaguana katika kusaidiana".
Amesema wafanyakazi wa sekta ya afya nchini Iran ni mashujaa na wako mstari wa mbele katika vita dhidi ya Corona lakini wanakabiliwa na uhaba wa vifaa muhimu vya kitiba na dawa. Katika ujumbe wake huo wa Twitter Zarif ameambatanisha orodha (tizama mwisho wa habari hii) ya mahitajio ya Wizara ya Afya ya Iran katika vita dhidi ya Corona. Vikwazo vya kidhalimu vya Marekani vimepelekea Iran isiweze kuagiza kutoka nje ya nchi vifaa na dawa znazohitajika katika vita dhidi ya Corona. Marekani pia imezuia Iran kununua kutoka nje ya nchi mali ghafi ya bidhaa hizo za kitiba.
Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif, amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisisitiza ulazima wa kuondolewa vikwazo haramu vya upande mmoja ilivyoekewa Iran na Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi ameeleza katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kwamba, katika barua hiyo, ambayo nakala yake imetumwa kwa wakuu wa jumuiya za kimataifa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote, Mohammad Javad Zarif ametilia mkazo ulazima wa kuondolewa vikwazo vyote vya upande mmoja, haramu na visivyo vya kisheria vya Marekani dhidi ya Iran ili kuweza kukabiliana na maradhi ya corona.
Wakati huohuo, mapema jana Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza katika ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, Tehran imeuomba Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) uipatie msaada wa fedha kwa ajili ya kupambana na kirusi cha corona kupitia fungu la "Wenzo wa Kifedha wa Haraka" Rapid Financial Instrument  lililotengwa na mfuko huo.
Hivi karibuni Mkurugenzi Mwendeshaji wa IMF, Kristalina Georgiev alitangaza kuwa, mfuko huo wa fedha wa kimataifa umetenga dola bilioni 50 kwa ajili ya kuzisaidia nchi zilizoathiriwa na maambukizi ya kirusi cha corona.
captcha