IQNA

Hali ya hatari duniani

WHO: Ugonjwa wa Corona, (COVID-19) umeenea duniani kote, maambukizi, vifo kuongezeka

23:07 - March 11, 2020
Habari ID: 3472555
TEHRAN (IQNA)- Hatimaye ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 umetangazwa kuwa sasa umeenea duniani kote (global pandemic), amesema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus.

Akizungumza na wanahabari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Dkt. Tedros amesema hatua ya kutangaza kuwa virusi vya Corona vimeenea duniani ni baada ya kubainika kuwa hadi sasa kuna zaidi ya wagonjwa 118,000 katika mataifa 114 ambapo tayari watu 4,291 wamefariki dunia.

“Maelfu wengine wako taabani hospitali wakihofia maisha yao. Katika siku na wiki zijazo, tunatarajia kuwa idadi ya wagonjwa itaongezeka, sambamba na idadi ya vifo na idadi ya nchi yenye wagonjwa halikadhalika. WHO imekuwa ikitathmini mlipuko na tumekuwa na hofu kubwa ya kuenea kwa ugonjwa huu na vile vile ukosefu wa uchukuaji  hatua,” amesema Dkt. Tedros.

Amesema ni kwa kuzingatia hilo wametathmni na kubaini kuwa COVID-19 sasa inaweza kuwa imeenea duniani kote.

Dkt. Tedros amekumbusha kuwa neno hilo ya kwamba umeenea duniani kote au kwa Kiingereza, Pandemic si neno la kutumia kwa urahisi tu au bila umakini. “Ni neno ambalo iwapo litatumika vibaya linaweza kusababisha hofu isiyotakiwa au watu kukubali bila sababu ya kwamba tumeshindwa kupigana vita dhidi ya ugonjwa vimekwisha na hivyo kusababisha machungu na vifo.”

3884850

captcha