IQNA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ajadiliana na wenzake wa Qatar na Uturuki kuhusu Afghanistan, corona

22:34 - April 13, 2020
Habari ID: 3472663
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na mawaziri wa mambo ya nje wa Uturuki na Qatar kuhusu matukio ya hivi karibuni kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini Afghanistan.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Habari ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana Jumatatu alifanya mazungumzo tafauti ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu  na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani ambapo wamejadili matukio ya Afghanistan na mchakato wa amani nchini humo.

Aidha mawaziri hao pia wamejadili kuhusu janga la corona katika eneo  na dunia nzima pamoja na njia za pamoja zinazoweza kutumika kukabiliana na janga hilo.

Siku ya Jumapili pia, Zarif alifanya mazungumzo ya simu na Hanif Atmar kaimu waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan.

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza kuhusu ulazima wa kuwepo umoja baina ya makundi mbali mbali ya Afghanistan pamoja na kuwepo amani na uthabiti na amani katika nchi hiyo huku akisisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa Tehran na Kabul.

Zarif aidha siku ya Jumapili alifanya mazingumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambapo aliwasilisha ripoti kuhusu jitihada za kidiplomasia za Iran za kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Afghanistan ili kufanikisha mchakato wa amani nchini humo.

3891364

captcha