IQNA

20:47 - March 16, 2020
News ID: 3472572
TEHRAN (IQNA) – Serikali ya Uturuki imepiga marufuku kwa muda sala za Ijumaa na jamaa katika misikiti nchini humo kutokana na hofu ya kuenea ugonjwa hatari wa COVID-19 maarufu kama kirusi cha corona.

Katika taarifa aliyoitoa Jumatatu, Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kidini Katika Ofisi ya Rais wa Uturuki (Diyanet), Sheikh Ali Erbas, amesema misikiti itabakia wazi kwa wale wanaotaka kuswali furada, yaani mtu kuswali peke yake pasina kuwepo jamaa.

Akizungumza na waandishi habari, Erbas amesema: "Hadi pale hatari ya kuenea kirusi kipya cha corona itakapotoweka, imekuwa dharura kusitisha sala za jamaa katika misikiti, hasa sala za Ijumaa."

Erbas aidha ametoa wito kwa waumini wajitahidi kuswali nyumbani. Hatua hiyo inakuja baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki kutangaza kuwa migahawa yote na maeneo mengine ya mijumuiko ya umma itafungwa nchini humo kuanzia Jumanne.

Aidha serikali ya Uturuki pia imefunga vyuo vikuu na shule huku ikipiga marufuku safari za ndege kutoka baadhi ya nchi. Halikadhalika maelfu ya raia wa Uturuki ambao wamrejea kutoka ibada ya Umrah nchini Saudi Arabia wamewekwa katika karantini. Kirusi cha corona huenea haraka katika maeneo ya umma hasa yenye mijimuiko mikubwa. Hadi kufikia Jumapili idadi ya walioambukizwa corona Uturuki ilikuwa ni watu 18.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, hadi kufikia 15 Machi, watu waliokuwa wameambukizwa COVID-19 kote duniani wamepindukia 152,428 huku waliofariki wakiwa ni zaidi ya 5,720 katika nchi 141 kote duniani.

3470932

Tags: corona ، msikiti ، uturuki
Name:
Email:
* Comment:
* captcha: