Akihutubia hafla hiyo Alhamisi, Sadiq alieleza kuwa ni baraka na heshima kubwa kushiriki katika mkusanyiko wa kiroho unaowakutanisha maqari kutoka nchi 36. Alisisitiza kuwa mashindano haya si tu maonesho ya ustadi wa tilawa, bali ni ishara ya nguvu ya umoja wa Ummah.
Spika huyo alimshukuru Waziri wa Masuala ya Kidini, Sardar Yusuf, kwa mwaliko, akisema mkutano huo unaakisi heshima ya pamoja ya Waislamu kwa Kitabu Kitakatifu. “Qur’ani Tukufu ni mwongozo kamili wa maisha, unaowaongoza wanadamu kutoka gizani hadi nuru,” alisema, akiongeza kuwa mafanikio ya dunia na Akhera hupatikana kwa kufuata mafundisho yake.
Aidha, aliwatakia kheri maqari wote waliokusanyika kutoka ulimwengu wa Kiislamu, akiwapongeza kwa kujitolea kwao katika sanaa ya tilawa.

Mashindano haya ya kwanza ya kimataifa ya Qur’ani nchini Pakistan yalianza Jumatatu, Novemba 24, yakihusisha washiriki kutoka nchi wanachama wa OIC. Yameandaliwa na Wizara ya Masuala ya Kidini kwa lengo la kuonyesha utamaduni na urithi wa kiroho wa taifa hilo, sambamba na kuimarisha uhusiano wa nchi za Kiislamu.
Mashindano haya pia yanakusudia kuwahimiza vijana kutafakari maana ya Qur’ani na kulinda urithi wa tilawa kwa vizazi vijavyo. Hafla ya kufunga mashindano itafanyika Novemba 29 katika Kituo cha Kimataifa cha Mkutano cha Muhammad Ali Jinnah, kwa kuhudhuriwa na viongozi wa kidini na serikali.
Miongoni mwa washiriki mashuhuri ni Adnan Momenin, qari maarufu kutoka Khuzestan, anayewakilisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
3495541